TANZANIA, KENYA  NA UGANDA KUWA MWENYEJI AFCON 2027

Habari njema kutoka Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF)limetangaza rasmi kuwa  nchi za tatu za Ukanda wa Afrika Mashariki; Tanzania, Kenya na Uganda zitakuwa wenyeji wa Afcon 2027.

Taarifa hiyo imetolewa rasmi Septemba 27, 2023 na Rais wa CAF, Dkt.Patrice Motsepe  nchini Misri katika Kikao Cha Kamati Tendaji ya Shirikisho kutoka katika kila nchi mwanachama Afrika.

Akizungumza katika kikao hicho, Dkt. Motsepe ameeleza mambo mengi muhimu yaliyozingatiwa kama vigezo vya kuzipitisha nchi hizi tatu kutoka Ukanda wa Afrika Mashariki kama yalivyoelezwa kwenye ripoti ya Kamati  Maalum iliyotumwa na CAF kuzitembelea nchi zote na kukagua baadhi ya hudumu za msingi kulingana na vigezo vya Shirikisho Hilo linalosimamia Soka Afrika.

Vigezo hivyo ikiwa ni pamoja na Miundombinu za Viwanja, Hoteli zilizopo,  upatikanaji wa Huduma ya Afya kama kuwepo kwa hospitali kubwa kwa ajili ya kutoa huduma za dharula zinapojitokeza kama inavyojulikana kuwa soka linahusisha kugongana uwanjani, usafiri na ubora wa Viwanja vya Ndege na kadhalika.

Ikumbukwe kwamba, mnamo Julai, 2023 Serikali kupitia Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo ilisema  Hospitali ya Taifa ya  MUHIMBILI imekidhi vigezo kushughulikia dharula za AFCON za kiafya  zinazoweza kujitokeza katika michuano ya Mpira wa Miguu Barani Afrika (AFCON 2027) ikiwa Afrika Mashariki itapewa ridhaa ya kuwa mwenyeji wa michuano hiyo.

Miongoni mwa maeneo yaliyokaguliwa ni pamoja na miundombniu ikiwemo viwanja vya Michezo, Hoteli, Viwanja vya Ndege na Hospitali mbalimbali kutoka nchi zote tatu.

Ukaguzi katika Hospitali ya Muhimbili ulihusisha   Idara ya Magonjwa ya Dharula na Ajali, mashine za kisasa za uchunguzi lakini pia wamepata maelezo mazuri kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili Prof. Mohamed  Janabi ambaye alielezea uwezo na utayari wa Hospitali hiyo kutoa huduma kwa ufanisi wakati wote wa michuano hiyo Mikubwa.

Kufanikiwa kwa “Pamoja Bid” kumekuja baada ya Serikali zote tatu kuridhia mpango huo ulioasisiwa na Mashirikisho matatu…TFF, KFF na FUFA ambao pia umepata baraka zote na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika CAF na kupatiwa fursa hiyo adhimu.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan alikutana na Ujumbe wa TFF ukiongozwa na Rais Wallace Karia kwa ajili ya kumkabidhi andiko la pendekezo la mpango huo ombi la kuandaa AFCON “Pamoja Bid” Mei 14 Ikulu, wakati FUFA wao walikabidhi Mei 15 halikadhalika KFF ambao nao walifanya hivyo mwezi Mei, 2023 pia.

Katika hatua nyingine, CAF imeridhia pia nchi ya Morocco kuandaa Michuano hiyo mwaka 2025, ambapo nchi hiyo imefanikiwa kukidhi vigezo vyote vilivyohitajika na CAF.

Nchi hizi za Afrika Mashariki ” Pamoja Bid” zilikuwa zikichuana na nchi nyingi zenye uzoefu mkubwa wa mashindano hayo kama vile Senegal, Botswana, Nigeria na Benin, Algeria, Afrika Kusini na Zambia.

Msafara wa Wajumbe waliokwenda Makao Makuu ya CAF Misri kwa ajili ya kushuhudia tukio hilo muhimu uliongozwa na Waziri mwenye dhamana ya Michezo Dkt. Damas Ndumbaro, Rais Wallace Karia, Makamu wa Kwanza wa Rais wa TFF Athumani Nyamlani, Mkurugenzi wa Sheria, Habari na Masoko wa TFF Boniface Wambura na Katibu wa Baraza la Michezo Tanzania Neema Msita ambao waliungana na Balozi wa Tanzania nchini humo Mhe. Dkt.Emmanuel John Nchimbi.