Tanzania Kenya na Uganda Mguu Sawa Kuwa Mwenyeji AFCON 2027

Timu ya Wakaguzi kutoka Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) imehitimisha ukaguzi Agosti 2, 2023 Visiwani Zanzibar kwa kufanya  kikao cha majumuisho kilichoongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Ndugu Saidi Yakubu.

Akizungumza katika kiakao cha majumuisho kilichofanyika Agosti 2, 2023 kwenye Hotel ya Hyat iliyopo (Stone Town), Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamadauni Sanaa na Michezo Ndugu, Yakubu Saidi alisema maeneo mengi yaliyokaguliwa yameowaridhisha wakaguzi licha ya kubainika kwa changamoto ndogo ndogo ambazo wamezitolea maelekezo ili mambo yawe sawa.

Katibu Mkuu Yakubu alifafanua maeneo yaliyokaguliwa na jopo hilo kutoka CAF kuwa ni; Uwanja wa Benjamin Mkapa uliopo Dar es Salaam, Uwanja wa Amani  Zanzibar, pamoja na Uwanja wa kufanyia mazoezi wa Mao TSE Tung ambao nao pia upo Zanzibar Mjini.

Miundo Mbinu mingine iliyokaguliwa ni Hospitali ya Rufaa ya Muhimbili na Mnazi Mmoja zote za Dar es Salaam, kadhalika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwl. Julius K. Nyerere pamoja na huduma nyingine Muhimu kwa mujibu wa vigezo vya CAF.

Akizungumza mara baada ya kikao hicho, Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania ambaye pia ndiye Rais wa CECAFA, Ndugu, Wallace Karia amezishukuru Serikali za nchi hizo kwa ushirikiano waliotoa kufanikisha ukaguzi huo ikiwemo nia thabiti ya kuomba kuwa wenyeji wa mashindano hayo makubwa Barani Afrika.

Rais Karia alisema kuwa ukaguzi huo umemalizika vizuri, na kwamba wakaguzi kutoka CAF wameona kuwa nchi hizi ziko makini na kwamba zina nia ya dhati ya kuwa mwenyeji, ambapo ameeleza kwamba kuna mambo ambayo wakaguzi hao wameelekeza ili yaweze kufanyiwa kazi.

Alisema kuwa kwa upande wa Tanzania Bara na Zanzibar yapo mengi yamefanyika kwa sababu wakandarasi wapo “site”na vitu vinaonekana; wameelekeza kuwa jambo hili lifanyike kwa pamoja huku wakitoa siku 10 kukamilisha nyaraka zote zinazohitajika kulingana na maelekezo yao.

Aidha, Rais Karia ametoa rai kwa mataifa yote matatu kutekeleza kwa pamoja maelekezo yaliyotolewa ili kufikia lengo la Afrika Mashariki kuandaa mashindano hayo ambayo hayajawahi kufanyika katika ukanda huo. Nchi hizo zinatakiwa kukamilisha miundombinu ya michezo itakayotumika kwenye mashindano hayo kabla ya Desemba 2025.

Hata hivyo, jopo hilo kutoka CAF limesema kuwa taarifa rasmi kuhusu ukaguzi huo itatolewa mara baada ya kukamilisha zoezi kama hilo linalotarajiwa kufanyika nchini Botswana siku za hivi karibuni (Agosti mwaka huu).

Wakaguzi hao kutoka CAF, hapa nchini Tanzania walipokelewa na Rais wa TFF na CECAFA Wallace Karia pamoja na Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni Sanaa na Michezo Ndugu Saidi Yakubu kwa niaba ya Serikali.

Jopo la viongozi kutoka nchi tatu; Tanzania, Kenya na Uganda linatarajia kukutana wiki ijayo Jijini Kampala Uganda kwenye kikao Maalum kujadili maelekezo yaliyotolewa Ujumbe huo kutoka CAF kuhusu suala hilohilo la maandalizi ya Michuano hiyo ya Afrika.