Timu ya Taifa ya Tanzania ya Soka la Ufukweni imeibuka na ushindi wa 6-4 dhidi ya Malawi katika michuano ya Copa Dar es salaam kuzidi kujihakikishia nafasi ya kutetea ubingwa wa michuano hiyo inayoendelea katika viwanja vya Coco.

Ushindi huo unaifanya timu hiyo kujikusanyia alama tatu ambazo zinafikisha jumla ya alama 6 baada ya kucheza michezo 3 mpaka sasa.

Magoli ya Tanzania yamefungwa na Jaruph Juma Rajab (2), Rolland N. Msonjo (2) , Juma Sultan goli moja na Yahaya Said Tumbo goli moja (1).

Kwa upande wa Malawi wafungaji ni Saandam Said Ussi (2), Ganizani Mphande jezi namba 11 (1) na James Chikoka jezi namba 6 naye akifunga goli (1) pia.

Kocha wa Tanzania Boniface Pawassa anasema siri ya mafanikio ya kikosi chake ni kuwatega Malawi na wao kukubali kuingia katika mtego huo bila kujijua; hali iliyopelekea wao kupata ushindi.

Hata hivyo Pawassa amesema kuwa kunamakosa ambayo wachezaji wake pia walikuwa wakiyafanya mara kwa mara jambo ambalo ameahidi kwenda kulifanyia kazi haraka leo na kesho asubuhi kabla ya kukutana na Burundi katika mchezo wa mwisho.

Pawassa amesema kuwa anauhakika wa asilimia tisini (90%) kukitetea kikombe chake kwa mara nyingine ili kuzidi kujitangaza vizuri katika mchezo huo kwa upande wa Africa.

Kwaupande wake Nahodha wa timu ya taifa ya Tanzania Jaruph Juma Rajab ambaye ndiye mfungaji wa goli la sita amesema kuwa mechi ilikuwa ngumu sana kwa kuwa wamecheza na timu ambayo haikuwa na alama hata moja; hata hivyo ameshukuru  kwa matokeo hayo na kuwataka mashabiki kufika kwaajili ya kuongeza hamasa ili waweze kupata ushindi zaidi.

Naye kocha wa Malawi ametupa lawama kwa waamuzi kuwa hawakuwa waungwana na kwamba wamekuwa wakiionea timu yake ambayo ilistahili kushinda.

Tanzania ikishinda kesho itakuwa na alama 9 ambazo haziwezi kufikiwa na timu yeyote hata kama Seychelles watashinda mechi Yao ya Leo bado hawataweza kufikisha alama 9, baadala yake watakuwa na alama 8 pekee katika michuano hiyo inayochezwa kwa mfumo wa ligi.