Tanzania yaanza vyema mashindano ya CECAFA U-18

Timu ya Taifa ya wanawake chini umri wa miaka 18 imeanza vyema mashindano ya CECAFA U-18 baada ya kupata ushindi wa goli 3-0 dhidi ya timu ya Burundi katika mchezo wa ufunguzi uliochezwa leo Julai 25 , 2023 katika uwanja wa Azam Complex, Chamazi majira ya sa 9 Kamili Alasiri.

Kipindi cha kwanza cha mchezo huo kilikua kigumu kwa timu ya Tanzania U-18 baada ya kuonyesha kuzidiwa na timu ya Burundi, lakini mabadiliko kadhaa yaliyofanywa katika kipindi cha pili yalizaa matunda yaliyopelekea Tanzania kubeba alama tatu.

Magoli ya Tanzania yalifungwa na Winifrida Gerald kwa mkwaju wa Penati Dk 64, na baadae DK ya 88 Sara Joel akatupia goli la pili akitokea benchi na Aisha Mnuka akakamilisha idadi ya magoli 3 katika dakika za nyongeza za kipindi cha Pili.

Akizungumza baada ya mchezo kumalizika kocha Bakari Shime alisema mechi ilikua nzuri licha ya kwamba wachezaji wake walicheza chini ya kiwango katika kipindi cha kwanza jambo ambalo alilifanyia kazi kipindi cha pili na timu ikaweza kurudi mchezoni na kutengeneza nafasi nyingi za kufunga.

“Lengo letu katika mashindano haya ni kuwa mabingwa lakini vilevile tutayatumia mashindano haya kama maandalizi ya kujiandaa na kombe la Dunia kwa wanawake chini ya umri wa miaka 20, hivyo hii ni sehemu sahihi ya kuona mapungufu yetu na kujirekebishia ili tuweze kufanya vizuri katika mashindano yajayo” alisema Kocha Shime.

Mechi nyingine iliyochezwa Leo Julai 25, 2023 ilikua Kati ya Ethiopia dhidi ya Uganda na ilimalizika kwa Uganda kubeba alama tatu baada ya ushindi wa goli 1-0 dhidi ya Ethiopia.