Tanzania yaichapa Ethiopia goli 2-0 Azam Complex, Chamazi

Timu ya Taifa ya Wanawake chini ya umri wa miaka 18 imeendeleza ubabe wake mara baada ya kuichapa timu ya Ethiopia goli 2-0 katika mashindano ya CECAFA U-18 yanayoendelea katika uwanja wa Azam Complex, Chamazi jijini Dar es Salaam.

Mchezo huo uliokuwa ukisubiriwa na wengi ulianza kwa Kasi katika kipindi cha kwanza huku timu zote zikionyesha kukamiana na kushambuliana kwa zamu. Tanzania ilimiliki mchezo Kwa asilimia kubwa na kufanikiwa kupata goli la mapema dakika ya 13 , goli likifungwa na nahodha wa timu Noela Luhala.

Goli la ushindi lilifungwa na Aisha Mnuka katika dakika ya 76 na Tanzania kufanikiwa kubeba alama 3 na hivyo kujikusanyia jumla ya alama 6 baada ya kushinda michezo yote miwili.

Akizungumza baada ya mchezo kumalizika kocha Bakari Shime alisema, ameridhishwa na kiwango cha wachezaji wake licha ya kwamba mchezo ulikua mgumu na Ethiopia kuonyesha ushindani mkubwa.

” Timu imekua na mwanzo mzuri na imecheza vizuri ukilinganisha na namna walivyocheza na Burundi, nina imani itaendelea kufanya vizuri katika michezo inayofuata kwani Lengo letu ni kutwaa ubingwa” alisema Kocha Shime.

Matokeo ya mechi ya mapema iliyopigwa saa 9 Alasiri Kati ya Uganda dhidi ya Zanzibar ilimalizika kwa Uganda kupata ushindi wa goli 3-0.

Mechi nyingine zitapigwa Julai 30, 2023 ambapo timu ya Ethiopia itacheza dhidi ya Burundi wakati mwenyeji Tanzania akivaana na timu ya Zanzibar.