Taifa Stars Yashindwa Kutamba Nyumbani Dhidi ya Intamba Murugamba’ ya Burundi
Mchezo wa kirafiki wa kalenda ya FIFA kati ya timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’na Burundi ‘ Intamba Murugamba’ imerindima leo tarehe 11 Oktoba, 2020 majira ya saa 10 jioni katika uwanja wa Mkapa Jijini Dar es Salaam ambapo Taifa Stars imeshindwa kutamba ikiwa nyumbani.
Mchezo huo uliokuwa ukisubiriwa kwa hamu na wapenzi, mashabiki na wadau wa soka nchini Tanzania kutokana na muda mrefu kupita tangu waishuhudie Taifa Stars ikiwa uwanjani; jambo lililosababishwa na kuzuka kwa janga la Corona lililopelekea shughuli zote za michezo kusitishwa.
Kipindi cha kwanza cha Mchezo kilianza kwa kasi ya aina yake ambapo Taifa Stars walionekana kuwa na moto na mashambulizi mengi yakielekea katika lango la Burundi, huku Burundi nao wakionekana kucheza kwa kuvizia wakitegemea zaidi mashambulizi ya kushtukiza .
Vuta ni kuvute ikaendelea huku timu zote mbili zikitunishiana misuli, kila moja ikitaka kumdhihirishia mwenzake kuwa imejipanga vilivyo kuondoka na ushindi; lakini licha ya ubabe huo mpaka kipindi cha kwanza kinamalizika si Tanzania wala Burundi aliyefanikiwa kuzitikisa nyavu za mwenzake.
Baada ya mapumziko, ngwe ya pili ilianza na Taifa Stars waliendelea kuonesha makali yao vilivyo, kwa kulisakama lango la Burundi mara kadhaa licha ya nafasi zote walizozipata kutokuzaa matunda. Burundi nao walikuwa macho wakijitahidi kuyazuia mashambulizi yaliyoelekezwa kwao wakijaribu kila namna ili kuzuia matokeo ya kupoteza mechi mara nyingi dhidi ya Tanzania.
Mabadiliko ya kutosha yalifanyika katika kipindi hiki kwa timu zote mbili ambapo mabadiliko hayo yalizaa matunda Kwa timu ya Burundi na kuweza kujipatia goli la 1 mnamo dakika ya 84; goli liliofungwa na mchezaji JN 10 aitwae Saidi Ntigamasambo.
Mechi hiyo ya Kirafiki ya kalenda ya FIFA ilimalizika kwa timu ya Burundi kuibuka na ushindi wa goli 1, goli lililopatikana katika dakika za lala salama.
Kocha wa Burundi Ndayizeye Jimmy alisema kuwa Kikosi chake kimejitahidi kufuata maelekezo yake kwa kucheza kwa kuiheshimu Taifa Stars na kufanya mashambulizi ya kushitukiza huku ikiyatumia vema makosa yaliyofanyika katika kipindi cha pili.
Kocha huyo alikisifia kikosi cha Tanzania kuwa kilicheza vizuri na kilishambulia sana hasa katika kipindi cha kwanza.
Naye kocha wa Taifa Stars Etienne Ndayiragije alisema kwamba kikosi chake kilicheza vizuri licha ya kukosa nafasi nyingi na za wazi, jambo ambalo kocha huyo alidai kuwa ni la kawaida katika soka.
Hata hivyo, Ndayiragije aliahidi kwenda kuyafanyia kazi makosa aliyoyabaini kupitia mchezo huo.
Mtanange huu wa kukata na shoka ulishuhudiwa na Waziri Mkuu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Majaliwa Kassim Majaliwa aliyekuwa mgeni rasmi pamoja na viongozi wengine wa kiserikali, lakini pia Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania TFF Wallace Karia aliyeambatana na katibu mkuu Kidao Wilfred nao waliushuhudia mtanange huu mwanzo mpaka mwisho.
Vikosi vilivyocheza katika mechi hiyo kwa upande wa wenyeji Taifa Stars ni; David Kisu (GK), Shomari Kapombe, Mohammed Hussein, Abdallah Kheri Bakari Ndondo, Jonas Mkude, Faisal Salum (Fei Toto), Said Hamis, Mbwana Samatta, Saimon Msuva na Iddi Sleman huku wa akiba wakiwa ni; Aishi Manula (GK), Metacha Mnata GK, Israel Mwenda, Nickson Kibambage, Dickson Job, Iddy Majaliwa, Salum Abubakar, Mzamiru Yassin, Ally Msengi, Thomas Ulimwengu na Ditram Nchimbi.
Burundi wao walikuwa na Onesime Rukundo GK, Erick Ndizeye, Fredrick Nsabiyaumva, Saidi Ntigama, Philip, zNimubona Emery, Steven Nzigamasabo, Saido Berahino, Cedrick Amissi na Mohamed Amissi. Wachezaji wa akiba walikuwa Jonathan Nahimana GK, Blaise Bigirimana, Blanchard Ngabonziza, Cedrick Urasenga, Ndikumana Asman, Hakizimana Issa, Bonfils Bimenyimana na Mugisha Alberto.
Mchezo huo ulimalizika kwa Taifa Stars kupoteza huku Jonas Mkude akioneshwa kadi nyekundu katika kipindi cha pili, tukio liloimaliza nguvu timu ya Tanzania baada ya kulazimika kucheza ikiwa na upungufu wa kiungo wake.