Want create site? Find Free WordPress Themes and plugins.

Tanzania yapoteza nafasi ya kufuzu BAFCON 2022

Timu ya Taifa ya Soka la Ufukweni “Beach Stars” imefanikiwa kuichalaza timu ya Taifa ya Malawi kwa jumla ya mabao 6-5 kwenye mchezo wa marudiano uliopigwa jijini Dar es Salaam katika Fukwe za “Coco” Julai 07, 2022 mnamo majira ya saa 9:30 alasiri.

Mchezo huo wa kukata tiketi ya kufuzu kushiriki AFCON ulikuwa ni muhimu kwa pande zote mbili na ulianza kwa kasi huku timu hizo zikishambuliana kwa zamu. Timu ya Malawi ndiyo iliyotangulia kuandika bao katika kipindi cha kwanza bao hilo likifungwa na mchezaji jezi namba (4) aitwae Isaac Kajam, bao ambalo halikudumu kwa muda mrefu kabla ya “Beach Stars” kuandika bao la kusawaziisha kupitia kwa mchazaji jezi namba (16) Stephan Mapunda. Dakika chache baadaye timu ya “Beach Stars” ilifanikiwa kuongeza bao la pili kupitia kwa Yahya Tumbo mwenye jezi namba (6) kabla ya Jaruph Rajabu (Jz10) kukomelea msumari wa 3 uliozipeleka timu hizo kwenye mapumziko huku ubao ukisoma 3-1.

Kipindi cha pili kilianza kwa nguvu na Tanzania ndio waliokuwa wa moto zaidi, wakipeleka mashambulizi mengi kwa Malawi yaliyowapatia bao la 4, lililofungwa na mchezaji Jaruph Rajabua aliye rejea kambani kwa mara ya pili huku bao la tano likipachikwa kimiani na Yahya Tumbo kabla ya Erick Manyama kugongelea nyundo ya sita na kuufanya mchezo huo kumilizika kwa bao 6-5.

Mabao mingine ya Malawi yalifungwa na Martin Biliati (Jz.5) aliyerudi kambani mara 2, Sandram Saddi (Jz. 10) huku bao la mwisho lililoinyong’onyeza timu ya Tanzania likifungwa na mchezaji jezi namba (11) aitwae Dala Simba.

Matokeo hayo yalizifanya timu hizo kulingana alama na idadi ya magoli 8-8 huku Malawi wakipata faida ya kufunga magoli mengi zaidi ugenini; jambo lililowapatia faida ya kusonga mbele kwa tofauti ya magoli ya nyumbani na ugenini.

Akizungumzia matokeo hayo kocha Msaidizi wa kikosi cha “Beach Stars” Deo Lucas alisema wao kama benchi la ufundi wamesikitishwa na matokeo hayo ambayo sio mazuri kwa ujumla. Aliongeza kuwa mchezo walikuwa wameushika lakini kwa bahati mbaya wachezaji walipoteza umakini zaidi kwenye dakika za lala salama; jambo lililopelekea timu yao kupoteza mchezo huo.

Aidha, Deo alisema licha ya kupoteza umakini kwa wachezaji wake kwenye dakika za mwisho, timu ya Tanzania haikuwa na bahati ya kusonga mbele kutokana na wao kuhimili takribani dakika 32 zote, kabla ya kuongezwa dakika moja. Hivyo, aliahidi kwenda kuyafanyia kazi makosa yaliyojitokeza kwenye mchezo huo ili kuweza kufanya vizuri na kufanikiwa kufuzu kwenda AFCON mwaka ujao 2023.

Mchezo huo ulikuwa ni wa kufuzu kushiriki michuano ya AFCON inayotarajiwa kuchezwa nchini Msumbiji-Mjini Maputo ifikapo Oktoba, 2022. Endapo timu ya Taifa ya Soka la Ufukweni “Beach Stars” ingefanikiwa kupata bao la saba ikawa 7-5 basi ingekuwa imefuzu kushiriki michuano hiyo. Lakini kutokana na ushindi wa 6-5 ikawa si Riziki tena.

Kikosi  kilichochezaji mchezo huo kiliundwa na;  Adam Oseja (JZ.13,GK), Erick  Manyama (JZ 5), Juma Sultani (JZ 4), Jaruph Rajab (JZ 10) na Yahya Tumbo (JZ 6). Wachezaji wa akiba walikuwa ni; Deoratius Munishi (JZ.18GK), Mtoro Nasoro (JZ.8), Sadick Max (JZ.2), Goodluck Gama(JZ.11), Abdilah Mohammed (JZ.3), Ibrahim Ibadi (JZ.7) na Stephan Mapunda (JZ.16) huku kikosi hicho kikiongozwa na kocha Mkuu Boniface Pawasa aliyekuwa akisaidiwa na Deo Lucas.

 

Did you find apk for android? You can find new Free Android Games and apps.