Tanzanite Queens Kukutana na Nigeria raundi ya tatu kufuzu Kombe la Dunia

Timu ya Taifa ya wanawake chini ya umri wa miaka 20 ‘Tanzanite’ imefanikiwa kusonga mbele katika raundi ya tatu ya kufuzu kombe la Dunia baada ya kuchapa timu ya Djibouti goli 7-0 katika mchezo wa marudiano uliochezwa katika uwanja wa Azam Complex, Chamazi.

Magoli ya ‘Tanzanite’ yalifungwa  na Jamila Rajabu aliyefunga magoli mawili sawasawa na Winifrida Gerald  huku Diana Mnaly, Zainabu Mohammed na Yasinta Mitoga wote wakifunga goli moja moja katika mchezo huo wa raundi ya pili uliochezwa majira ya Saa 10 kamili jioni.

Akizungumza baada ya mchezo huo kumalizika Kocha Msaidizi wa Timu ya ‘Tanzanite’ Ester Chabruma alisema, ” Mchezo wa raundi ya pili umemalizika na tunamshukuru  Mungu kwa ushindi mnono tulioupata. Ushindi huu umetuongezea nguvu ya kupambana zaidi  kuelekea katika mchezo wa raundi ya tatu dhidi ya Nigeria.

“Tunakwenda kuimarisha Kikosi na kurekebisha mapungufu yaliyoonekana katika  mchezo dhidi ya Djibouti kama ilivyowezekana kwa timu ya ‘Serengeti Girls’ kucheza kombe la Dunia 2022 basi inawezekana kwa timu ya Tanzanite kutupeleka Columbia katika Fainali za Kombe la Dunia mwaka 2024” alisema Chabruma.

Tanzanite Queens inasonga mbele kwa jumla ya mabao (12-0) baada ya kuifunga Djibouti goli (5-0) katika mchezo wa kwanza Oktoba 8,2023  na kuifunga tena katika mchezo wa marudiano Leo Oktoba 11, 2023 goli (7-0), Michezo yote miwili ikichezwa nchini Tanzania katika uwanja wa Azam Complex.