Tanzanite Queen’s Yarejea Nyumbani Ikitabasamu

Kikosi cha timu ya Taifa ya wanawake  wenye umri chini ya miaka 20 (U-20) kimerejea Leo Septemba 28, 2021 kikitokea nchini Eritrea walipokwenda kucheza mchezo dhidi ya wenyeji ‘Eritrea’ ikiwa ni katika harakati za kuwania kufuzu kushiriki Kombe la Dunia ambapo Tanzanite Queen’s walifanikiwa kuianza vyema safari yao kwa kuibuka na ushindi mnono wa bao 3-0  katika uwanja wa Asmara nchini humo.

Akizungumza mara baada ya kuwasili katika uwanja wa kimataifa wa ndege wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere Kocha msaidizi wa timu hiyo Edna Lema alisema, anamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kupata matokeo mazuri ugenini.

Kocha Edna alieleza na kusema kuwa bado safari inaendelea, kwani lengo lao halikuwa kushinda mechi moja ya Eritrea tu, bali wanataka kushinda kila mchezo na kuweza kupata tiketi hiyo ya kushiriki Kombe la Dunia kwa mwaka 2022 huko Costa Rica.

Kocha huyo aliwataka watanzania wote kuzidi kuoimbea timu hiyo ya Tanzanite na kuipa ushirikiano huku akiwaahidi kwamba kikosi chake kitafanya vizuri kutokana na maandalizi waliokuwanayo hapo awali; vile vile, maandalizi wanayokwenda kuyaanza mara baada ya kurejea nchini Tanzania.

Naye nahodha wa timu ya Tanzanite Queen’s Irene Kisisa alisema kuwa mchezo wao dhidi ya Eritrea ulikua mgumu lakini waliweza kufanya vizuri kutokana na maaandalizi mazuri nay a muda mrefu waliokuwanayo pamoja na kuzingatia mambo yote waliyofundishwa na waalimu wao.

Nahodha huyo alitanabaisha ya kuwa pamoja na maandalizi waliokuwanayo bado   jitihada, kujituma na kujiamini ndiko kulikopelekea wao kupata matokeo mazuri ugenini. Hivyo, akawaomba  watanzania pamoja na wadau wa soka  kuendelea kuwa na imani na kikosi chao kwa kuwa kimejiandaa vyakutosha na kwamaba hakitawaangusha katika mchezo wa marudiano ambao utakwenda kupigwa Oktoba 9, 2021 hapa jijini Dar es salaam.

Wachezaji waliofunga magoli katika mchezo dhidi ya Eritrea ni Aisha masaka aliyefunga magoli 2 wakati Clara Luvanga akifunga goli 1 na kufanya jumla ya magoli yaliyopatikana katika mchezo huo wa kufuzu kushiriki Kombe la Dunia  kukamilika kwa 3-0.

Michuano ya Kombe la Dunia kwa wanawake wa U-20 ilianza kufanyika rasmi mwaka 2002 ikijumuisha nchi wanachama wa FIFA hivyo kwa mwaka 2022 itakuwa ni mara ya  kumi kufanyika baada ya kushindwa kufanyika mwaka 2020 kutokana na kuzuka kwa ugonjwa wa Uviko_19, na hii itakuwa mara ya pili kwa nchi ya Costa Rica kuwa mwenyeji wa michuano hiyo baada ya mara ya mwisho kufanyika nchini humo mwaka 2014.