Tanzanite VS Ethiopia Leo

Mchezo wa marudiano kati ya timu ya taifa ya wanawake chini ya miaka 20 “Tanzanite” dhidi ya timu ya wanawake chini ya miaka 20 ya Ethiopia unatarajiwa kupigwa leo majira ya sa 10:00 jioni katika Dimba la Abebe Bikila-Addis Ababa nchini Ethiopia ikiwa ni katika harakati za kuwania kufuzu kushiriki kombe la dunia (U-20) mwaka huu nchini Costa Rica.

Akizungumza kuelekea mchezo huo kocha mkuu wa Tanzanite Bakari shime alisema “anamshukuru Mungu kwa kuwafikisha salama Ethiopia na mpaka sasa hakuna majeruhi yoyote katika kikosi chake na wachezaji wote wako tayari kwa mchezo”.

Shime hakuacha kugusia kuhusiana na hali ya uwanja alivyouona akisema kwamba “kiwanja kinaonekana kimetumika sana na hakina ubora wa kuridhisha kwa ajili ya mchezo lakini hilo halitakuwa kikwazo kwao kwani kikosi kimejiandaa kucheza katika mazingira yoyote, vile vile changamoto ya baridi na uwazi wa uwanja unaosababisha hewa kuingia kwa wingi, lakini wamejipanga kukabiliana nayo na mwisho wa siku waweze kupata matokeo mazuri yatakayowapa nafasi ya kuendelea katika hatua ya tano na mwisho”.

Akizungumza kwa niaba ya wachezaji wenzake Asha juma alisema mchezo wa leo ni wa muhimu sana kwao na unakwenda kuweka historia kubwa kwao kama kikosi lakini pia kwa watanzania wote, ni mchezo utakaoamua hatima yao kama wataendelea mbele ama wataishia hapo.

Kwa upande wa maandalizi kila kitu kiko sawa na wamefanya marekebisho katika makosa yaliojitokeza katika mchezo wa hapa nyumbani dhidi ya Ethiopia mchezo uliochezwa siku ya jumapili ya tarehe 23 januari, 2022 katika Dimba la Amani Visiwani Zanzibar, hivyo watanzania waendelee kuwaamini na kuwaombea ili waweze kupata ushindi katika mchezo wa leo.

Kikosi cha Tanzanite kiliondoka nchini Tanzania siku ya tarehe 2 Februari, 2022 kikitokea Karatu jijini Arusha mahali ambako walipiga kambi kwa ajili ya kujionia dhidi ya Ehiopia.