Tanzanite Kucheza Mechi ya Kirafiki Dhidi ya Uganda Siku ya Uhuru, Disemba 9

Timu ya Taifa ya wasichana wenye umri chini ya miaka 20 (Tanzanite) inatarajia kushuka dimbani Disemba 9, 2021 kwenye sherehe za maazimisho ya miaka 60 ya Uhuru wa Tanganyika kucheza mchezo wa kirafiki ya Kimataifa dhidi ya timu ya Taifa ya wasichana (U20) kutoka nchini Uganda.

Taarifa hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Baraza la Michezo Omary Yusuph Singo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari za michezo kwenye mkutano uliofanyika Disemba 7, 2021 katika ukumbi wa mikutano uliopo uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam.

Taarifa hiyo iliyotolewa na Mkurugenzi Singo ililenga kuwafahamisha mambo mabli mbali yanayoendelea kwa upande wa Serikali hususani Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kuelekea maazimisho ya miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania Bara (Tanganyika).

Singo alisema kuwa Serikali kupitia Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa kushirikiana na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na Azam Media Limited zimeandaa michezo ya kirafiki ya Kimataifa maalum kwa ajili ya siku hiyo ya Disemba 9.

Alisema kuwa hapo awali ilikuwa inafahamika kuwa ni Taifa Stars pekee ndio itakuwa na mchezo huo wa kirafiki dhidi ya timu ya Taifa Uganda, lakini kufuatia taarifa hiyo iliyotolewa ni wazi kuwa kutakuwa na michezo miwili; mchezo wa kwanza utachezwa majira ya saa 11 jioni kati ya Tanzanite na Uganda na baadaye kufuatiwa na mchezo wa Taifa Stars dhidi ya Uganda utakuopigwa kuanzia saa mbili usiku. Michezo yote hiyo itapigwa kwenye dimba la Benjamin Mkapa.

Mbali na hayo, Singo alieleza kuwa lengo hasa la kupanga mechi hizo kuchezwa muda huo ni kutaka watanzania kusherehekea pamoja na kuweza kujumuika kupata mahali pa kupumzika au kupumzisha akili mara baada ya kukamilisha majukumu mengine ya kujenga Taifa.

Kupitia mkutano huo na waandishi wa habari, pia Singo alitaja viwango vya viingilio ambavyo alidai ni vya kawaida na kwamba vitamuwezesha Mtanzania wa ngazi yoyote kuweza kuviumudu na kujumuika pamoja kupata burudani kwa kutazama mitanange hiyo.

Alisema kuwa bei za viingilio hivyo zitakuwa ni elfu mbili (2,000) Mzunguko, elfu tatu (3,000) VIP A na B, halikadhalika kwa VIP ambapo itakuwa ni shilingi elfu tano (5,000) fedha za Kitanzania.

Vile vile, Mkurugenzi huyo aliwashukuru TFF na Azam Media Ltd. kwa ushirikiano wao katika kuhakikisha mambo yanakamilika na kuwa kama jinsi matarajio yao yalivyokuwa. Katika Mkutano huo TFF yeyewe iliwakilishwa na Katibu Mkuu Kidao Wilfred ambaye ndiye msimamizi wa shughuli za kila siku za Shirikisho.

Kuelekea maandalizi ya mechi hizo mbili, timu zote tayari zipo kambini zikiendelea na mazoezi ya kujiweka sawa kwa ajili ya hiyo huku Serikali, TFF na Azam Media wakiendelea na maandalizi mengine ili kuhakikisha kila kitu kinakuwa sawa na michezo hiyo inafanyika kwa ufanisi mkubwa. Kwa upande wa timu waalikwa kutoka Uganda zenyewe zinatarajia kuwasili nchini Tanzania Disemba 8, 2021.