Tanzanite Yaanza Vyema Safari Kulekea Costa-Rica 2022

Mchezo wa kuwania kufuzu kushiriki Kombe la Dunia kati ya timu ya Taifa ya Tanzania “Tanzanite” na Burundi umemalizika kwa Tanzanite kuibuka na ushindi wa mabao 3-2, kwenye mchezo wa kwanza uliopigwa Desemba 4 saa 9:00 alasiri katika uwanja wa Azam Complex uliopo Chamazi Mbagala Jijini Dar es Salaam.

Mchezo huo ulikuwa na upinzani mkali kwa timu zote ambapo timu ya Tanzania ilifanya mashambulizi ya haraka haraka kwenye kipindi cha kwanza na kufanikiwa kufunga mabao mawili ya mapema. Bao la kwanza lilifungwa na mchezaji Clara Luvanga (7) kunako dakika ya tisa (9) ya mchezo kabla ya Joyce Lema kuongeza bao la pili mnamo dakika ya 15.

Timu ya Burundi iliamka na kuanza kupeleka mashambulizi mfululizo na hivyo kuisababishia Tanzanite kufanya makosa mengi yaliyopelekea Waburundi hao kupata bao la kwanza dakika ya 21, bao hilo likifungwa na mchezaji Estellah Gakima wakati bao la tatu la Tanzanite lilipachikwa nyavuni na mshambuliaji hatari wa timu hiyo Aisha Khamis Masaka dakika ya 41 na kuyafanya matokeo kuwa 3-1mpaka timu hizo zinakwenda kwenye mapumziko.

Kipindi cha pili kilianza ambapo mtanange ulishika kasi huku timu zote zikiendelea kushambuliana kwa zamu. Kunako dakika ya 61 ya mchezo huo timu ya Burundi ilifanikiwa kuandika bao la pili kupitia kwa mchezaji Noela Izakoze (14). Bao hilo lilifanya mchezo kutamatika kwa tofauti ya mabao 3-2.

Kocha Bakari Shime baada ya mchezo huo alisema kuwa anashukuru kumaliza mchezo salama licha ya kupata majeruhi kadhaa akiwemo golikipa Husna Zuberi. Alieleza kuwa mchezo huo haukuwa mzuri kwa upande wao kutokana na kushindwa kulinda magoli ambayo waliyapata katika kipindi cha kwanza.

Mbali na hayo kocha Shime alisema wachezaji wake hawakuwa makini na walipoteza kila kitu kutokana na presha iliyokuwepo kutoka kwa wapinzani wao Burundi, hivyo alikiri kuwa matokeo ya  mchezo huo hayakuwa mazuri na kwamba wanakazi ngumu kwenda kuhakikisha wanapata matokeo ya ugenini.

Kwa upande wa kocha wa Burundi Mijibimenye Daniella alisema kuwa mchezo huo ulikuwa mzuri licha ya kupoteza kwani katika kipindi cha kwanza walikosa umakini na kuruhusu mabao mawili ya haraka yaliyowatoa mchezoni na hivyo kuanza kucheza kwa wasiwasi bila maelewano.

Aliongeza kuwa baada ya kwenda mapumziko aliwaeleza wachezaji wake watulie na kucheza mpira kwani kila kitu kinawezekana, jambo ambalo lilileta ufanisi na kupelekea kupata bao la pili na hivyo kuwa wameifanya kazi ya mchezo wa pili kuwa nyepesi kwao.

Tanzania watasafiri siku chache zijazo kwenda Burundi kucheza mchezo wa marudiano Desemba 18 na mshindi wa jumla atakutana na mshindi kati ya Ethiopia na Botswana. Mshindi wa hapo atakuwa amekata tiketi ya kwenda Kombe la Dunia nchini Costa Rica 2022.

Tanzania wanahitaji ushindi au sare ya namna yoyote ili kukata tiketi hiyo ya Kombe la Dunia, wakati Burundi watatakiwa kushinda kuanzia goli moja tu ili wasonge mbele kutokana na mtaji wa mabao mawili waliyopata ugenini.