Tanzanite Yashindwa Kutamba Mechi ya Kirafiki

Timu ya Taifa ya wasichana chini ya miaka 2O (Tanzanite) yashindwa kupata matokeo mbele ya timu ya Taifa ya Uganda baada ya kupoteza kwa bao 1-0 kwenye mchezo wa kirafiki uliopigwa kwenye dimba la Benjamin Mkapa Disemba 09, 2021 majira ya saa 10:30 jioni.

Mchezo huo ukiwa ndio wa kwanza kupigwa kati ya mechi mbili za kirafiki zilizopigwa kwenye sherehe za Uhuru wa Tanganyika ulianza ukionekana na kutokuwa na maelewano kwa timu ya Tanzanite, hali iliyopelekea kuwapa faida Uganda ambao walitumia nafasi hiyo na kupata bao la mapema mnamo dakika ya 18 kipindi cha kwanza likifungwa na Khadija Nandago (JZ 12).

Licha ya Tanzanite kuwa nyuma kwa bao moja mpaka kipindi cha kwanza kinamalizika bado haikuwa sababu ya wao kufanya vibaya dakika 45 za kipindi cha pili ambapo walionekana kurudi wakiwa bora zaidi kwa kucheza pasi nzuri zilizo na maelewano hivyo kumridhisha kocha kwa kiwango hicho walichokionesha.

Baada ya mchezo huo kumalizika makocha wa timu zote waliweza kuzungumza ambapo kocha wa Tanzanite Bakari Shime alisema kuwa licha ya wao kupoteza kwenye mechi hiyo jambo muhimu ni kiwango alichokiona kwenye kikosi chake kwa ubora kilichouonesha ukilinganisha na mechi yao ya mwisho waliyocheza Disemba 04 dhidi ya Burundi. Kwani, inaonesha wazi kuwa kuna mabadiliko ya kuridhisha kwenye kikosi hicho.

Aidha, aliweka bayana furaha yake kwa kupata nafasi ya kucheza mechi hiyo ikiwa na maana kubwa kwao kuweza kufahamu makosa kabla ya kwenda kucheza mechi yao ya marudiano Disemba 18, 2021 nchini Burundi. Mchezo huo dhidi ya Burundi ni katika kusaka tiketi ya kushiriki Kombe la Dunia 2022  huko Costa Rica.

Kwa upande wa kocha mkuu wa Uganda Ayub Khalifa aliwapongeza Tanzanite kwa mchezo mzuri na kusema ushindi wao ni kutokana na uwezo wao wa kutumia vizuri nafasi walizozipata; kitu ambacho kwa Tanzanite hakikuwa rahisi. Hivyo, ni kipimo cha timu yake kabla hawajakutana na timu ya Taifa ya Afrika Kusini kwenye mashindano ya Kufuzu Kombe la Dunia.

Ikumbukwe mchezo huo uliopigwa jioni ya kilele cha siku ya kufikisha miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania Bara. Mchezo huo ulikuwa ni sehemu ya Taifa la Tanzania kuweza kujumuika kwa pamoja na mataifa jirani katika kusherehekea Uhuru na mafanikio mbalimbali ya Taifa na mtanzania mmoja mmoja tangu kupatikana kwa Uhuru, ambapo sherehe hizo zilianza usiku wa kuamkia siku hiyo.

Kikosi kilichoanza kwa Tanzanite; Janeth Shija(GkJN20), Emiliana Isaya(JN 15), Fumukazi Ally( JN 04), Christer John (JN 17), Violeth Nicholus(JN 21), Esther Mabanza( JN 05), Protasia Mbunda (JN 03), Irene Kisisa(JN 19), Aisha Masaka(JN 10), Aisha Juma(JN 09) na Clara Luvanga( JN 07).

Na kikosi cha Uganda kilichoanza; Nyaenga Daphine(GK JN 01),Komuntale Sumaya(JN 03), Nadunga Bira(JN 17), Nakibuuka Asia(JZ 23), Nantongo Aisha(JN 05), Nandege Zainah (JN 20), Ninyagahirwa Shakira( JN 08), Najjemba Fauzia(JN 13) na Nakaiwa Samalie(JN 09), Nandago Hadija(JN 12) na Kunihira Magreth (JN 14).