Tanzanite Yazima Ndoto za Eritrea Kibabe
Timu ya Taifa Tanzania ya wanawake wenye umri chini ya miaka ishirini (U20) ijulikanayo kwa jina la ‘TANZANITE’ imefanikiwa kuifunga timu ya Eritrea kwa mara nyingine tena mara baada ya kufanya hivyo katika mchezo wa kwanza uliopigwa nchini Eritrea Septemba 25 2021 ambapo timu hiyo iliwalaza kwa jumala ya bao 3-0 kabla ya kurudia kufanya hivyo kwenye mchezo wa marudiano ambao Tanzanite imeibuka na ushindi wa bao 2-0.
Mchezo marudiano wa kufuzu kushiriki kucheza Kombe la Dunia 2022 huko Costa Rica, kati ya timu hizo uliopigwa Oktoba 09, 2021 kwenye uwanja wa Azam Complex Chamazi mnamo majira ya 9:00 Alasiri uliifanya safari ya timu ya Eritrea kukoma, mara baada ya kupokea kipigo cha bao mbili kwa sifuri na kuifanya timu ya Tanzanite kufikisha magoli matano kwa bila (5-0); matokeo yalizamisha moja kwa moja Jahazi la Eritrea na hivyo kuipatia nafasi Tanzanite kusonga katika hatua nyingine inayofuata.
Katika mchezo huo wa marudiano uliopigwa Tanzania Oktoba 09, Tanzanite iliingia uwanjani ikiwa na mtaji wa bao 3-0 yaliyopatikana katika mchezo wa awali; jambo lililowapa matumaini wachezaji wa kikosi hicho walioingia mchezoni huku wakijiamini, licha ya ugumu waliokutana nao katika kipindi cha kwanza ambapo mchezo huo ulimalizika pasipo timu yeyote kuandika bao kwa dakika zote 45.
Kipindi cha pili mambo yalibadilika huku kila timu ikiwa imefanya mabadiliko ya hapa na pale kwenye kikosi chake; Tanzanite ilimtoa Vironoca Mapunda (Jembe 23) na kumuingiza Protesia Mbunda (3) kabla ya kumtoa Joyce Lema na kumuingiza Diana William. Wakati kwa upande wa Eritrea wao walimtoa Venus Habte nafasi yake ikichukuliwa na Rahel Michael huku Deline Sahle akiingia naye kuchukua nafasi ya Yordanos Abraham.
Mabadiliko hayo yaliwasaidia wote huku Tanznaite wao wakinufaika zaidi, kwani wachezaji walioingia waliongeza mashambulizi zaidi na kuifanya Tanzanite kuandika bao lake la kwanza mnamo dakika 54 likifungwa na Irene Elias Kisisa(C-19) na bao la pili likifungwa na ‘supa sabu’ (Super Sub) Protesia Pius Mbunda; goli ambalo liliufanya mchezo huo kumalizika kwa Tanzanite kuibuka kidedea kwa bao 2-0. Mabao hayo yanaifanya Tanzanite sasa inakuwa na jumla ya magoli 5-0 ukijumuisha na yale walioshinda katika mchezo wao wa awali uliopigwa nchini Eritrea Septemba 25.
Akizungumza na waandishi wa habari za michezo baada ya mchezo huo, kocha Edna Lema alisema mchezo huo ulikuwa mgumu licha ya ushindi walioupata; kwani wapinzani wao waliingia kwa mbinu ya kujilinda zaidi na hivyo kuifanya safu yake ya ushambuliaji kutabika namna ya kuivuka ngome iliyokuwa imewekwa na Eritrea. Edna aliongeza kwa kuwashukuru wachezaji wake kwa kazi kubwa walioifanya kuhakikisha wanapata matokeo, tangu kwenye mchezo wa ugenini na katika mchezo wao wa pili ambao pia ulikuwa na umuhimu mkubwa kwa kuwa walihitaji zaidi kushinda katika ardhi yao ya nyumbani.
Kwa upande wake kocha wa Eritrea Ghezai Tesfagabir amekubali matokeo na kusema kuwa kikosi chake kimepambana kadri kilivyoweza lakini wamekutana na timu ngumu na bora ambayo ilistahili kupata matokeo iliyoyapata. Hata hivyo, kocha huyo alikipongeza kikosi cha Tanzanite kwa kuonesha mchezo mzuri huku akikumbushia mapokezi na ukarim aliooneshwa na viongozi wa mpira wa Tanzania.
Ikumbukwe kuwa timu ya Eritrea ilifanikiwa kufika katika hatua hiyo ya pili baada ya kuondoa Djibouti kwa bao 3-0 kwenye mchezo uliopigwa Agosti 18, 2021 huku ikisonga mbele kwa tofauti ya bao 6-1 dhidi ya Djibouti, na sasa imekuja kukumbana na kisiki cha Tanzanite kilichoifanya timu hiyo iliotinga hatua hiyo kwa kishindo kushindwa kutamba katika michezo yote miwili nyumbani na ugenini na baadala yake kuabulia kipigo cha bao5-0 kilichokatiza safari yake ya kushiriki Kombe la Dunia 2022 huko Costa Rica.