TFF, CRDB Zasaini Mkataba “CRDB Federation Cup”
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania TFF limeingia makubaliano na benki ya biashara (CRDB Bank) Kwa Kusaini mkataba wa miaka mitatu unaogharimu shilingi Bilioni 3.76 za Tanzania unaoupatia ridhaa benki hiyo kudhamini mashindano ya Kombe la Shirikisho Kwa muda wa miaka mitatu na nusu.
Mkataba huo umesainiwa Aprili 2, 2024 makao makuu ya CRDB jijini Dar es salaam, sambamba na kuyapatia jina jipya mashindano hayo baada ya makubaliano ya pande zote mbili yatakayo itwa (CRDB Bank Federation Cup).
Akizungumza wakati wa hafla hiyo fupi ya utiaji Saini Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Abdul Majid Nsekela, alisema kwao ni nafasi na bahati kubwa kushirikiana na TFF kwani Kwa muda mrefu wamekuwa wakitamani kupata nafasi hiyo adhwimu hasa katika Soka hapa nchini.
“Benki yetu ni mdau mkubwa wa michezo nchini, tumekuwa tukishirikiana na wadau mbalimbali wa Mpira, lakini sasa tumeona ndio wakati sahihi wa sisi kushirikiana na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania TFF katika kuendeleza kile kinachofanywa na Rais Wallec Karia” alisema Nsekela.
Kwa upande Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania TFF Wallec Karia alisema wanayo furaha ya kuingia makubaliano hayo na benki ya CRDB ambao ndio wamekuwa wadhamini wakuu wa kwanza kwenye mashindano hayo tangu yameanza.
“Adhima ya TFF ni kuzidi kuimarisha vipaji vya Mpira kupitia mashindano mbalimbali, tuna mashindano mengi kuanzia ngazi za wilaya mpaka ligi kuu yote tunayosimamia na kuendesha kama walezi wakuu wa mpira wa Miguu nchini ” alisema Rais Karia.
Hata hivyo fedha za mkataba huo zitaelekezwa kwenye maeneo muhimu zaidi, ambapo zitalenga zawadi mbalimbali zinazotolewa baada ya mashindano kama Kombe Kwa timu bingwa, tuzo zitolewazo Kwa timu na wachezaji bora kwenye kila maeneo na hata Ile timu bora Kwa misimu yote mitatu ya udhamini.
Aidha Rais Karia alisema Kupitia kikao chao Cha mwisho Cha kamati tendaji ya TFF kimekubaliana kuwa mchezo wa hatua ya fainali Kwa msimu huu utachezewa mkoa wa Manyara kwenye uwanja wa Tanzanite huku nusu fainali moja kupigwa Mwanza na nyingine itapangwa baada ya kufikia muafaka wa majadiliano yanayoendelea.
Hafla hiyo fupi ya utiaji Saini umeshuhudiwa pia na viongozi mbalimbali kutoka TFF; makamu wa Kwanza wa Rais TFF Athumani Nyamlani, Makamu wa pili wa TFF Steven Mnguto, Katibu mkuu wa TFF Kidao Wilfred, Afisa mtendaji Mkuu wa Bodi ya ligi(tplb) Almas Jumapili Kasongo, pamoja na viongozi wengine wa TFF na CRDB.