Want create site? Find Free WordPress Themes and plugins.

TFF na Precession Airline Zaingia Mkataba

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limeingia makubaliano ya kimkataba na Shirika la Ndege la “Precession Air” wa kuwa Msafirishaji rasmi  wa Kombe la Shirikisho linalojulikana kama (Azam Sports  Federation Cup).

Mkataba huo uliosainiwa na pande mbili Novemba 2, 2022 kwenye Hoteli ya  Diamond Plaza Jijini Dar es Salaam, unathamani ya zaidi ya milioni Mia moja (100,000,000)  za Kitanzania utakao dumu kwa mwaka mmoja; kuanzia 2022 hadi 2023.

Akizungumza katika tukio hilo la kihistoria, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Ndege la “Precession Air-line” Patrick Mwanri alisema kuwa wameamua kudhamini kilipo kitovu cha Soka kwani hapo awali walikuwa wakidhamini timu za pembeni pembeni, tofauti na sasa ambapo wameamua kwa dhati kujitokeza rasmi ili kuongeza tija kwenye soka,TFF na Serikali kwa ujumla.

Mwanri aliongeza akisema kudhamini Kombe hilo ni kuiunga mkono TFF katika kurahisisha  utekelezaji wa majukumu yake, ambapo alidai kuwa sababu nyingine ni utendaji na usimamizi madhubuti wa rasilimali fedha ambapo wamebaini kuwa viongozi waliopo wamekuwa wakielekeza fedha zote kwenye matumizi ya maendeleo ya soka nchini. Jambo hilo lilimewatia moyo na hivyo kuamua kuwekeza huku wakiamini fedha hizo zitakuwa salama.

Mbali na hayo, Mkurugenzi huyo alibainisha kuhusu juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita iliyo chini ya Rais Samia Suluhu Hassan ambayo imekuwa ikijitoa kwa hali na mali katika kuzisaidia timu za taifa na kuhamasisha wadau mbalimbali kujitokeza na kudhamini soka la Tanzania kama sehemu ya kutengeneza na kuongeza ajira kwa Watanzania hususani wachezaji.

Akitoa shukrani kwa niaba ya TFF,  Rais Wallace Karia aliushukuru uongozi wa Shirika la Ndege la “Precession Air” kwa kutambua juhudi ambazo Shirikisho hilo limekuwa likizifanya ili kuhakikisha mpira wa Tanzania unakua na kuimarika zaidi. Alisema hiyo ni dalili njema na kwamba wao kama wenye dhamana ya kusimamia shughuli zote za soka nchini wanafarijika kuona wadhamini wanakaribia na kushirikiana nao katika kuhakikisha malengo waliojiwekea yanatimia tena kwa wakati.

Rais Karia aliongeza kuwa udhamini huo hautakomea hapo bali unaweza kujitanua zaidi hapo baadaye na kudhamini pia Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB). Wao kama Shirikisho bado wana uhitaji mkubwa wa wadhamini. Aidha, Rais Karia alitaja bidhaa nyingine zinazohitaji udhamini kama vile; Ligi ya Mabingwa wa Mikoa (RCL) Ligi za vijana U17 na U20, pamoja na Ligi za Wanawake halikadhalika Championiship Ligi na Ligi Daraja la Kwanza pia.

 

Did you find apk for android? You can find new Free Android Games and apps.