TFF yaendesha kozi ya Grassroots.

Rais wa shirikisho la mpira wa miguu Tanzania Wallace Karia amefungua kozi ya awali ya ukocha wa Grassroots “FIFA GRASSROOTS FOOTBALL COACHING COURSE” inayofanyika makao makuu ya TFF Karume jijini Dar Es Salaam.

Kozi ya Grassroots ni mahususi kwa makocha wote wenye mataraijio ya kufundisha watoto wadogo kuanzia umri wa miaka 4-12 ambapo inaaminika kuwa ni muda sahihi wa kuvijenga vipaji vya watoto katika mpira kwani akili za watoto kwa wakati huo huwa tayari kupokea vitu vipya na ni rahisi kuvishika

Akifungua kozi hiyo rais Karia aliwataka washiriki kuona umuhimu wa mafunzo yanayotolewa na TFF na kwenda kuyafanyia kazi ili hapo baadae matunda yaweze kuonekana kwa kuwa uhitaji wa makocha hapa nchini bado ni mkubwa katika kuhakikisha vipaji vya soka vinaibuliwa kutoka pande zote za Tanzania ili kukuza zaidi soka letu kwa ngazi za vilabu na timu za Taifa.

Mbali na hayo Karia alifurahishwa na mwitikio mkubwa wa washiriki wa kike Katika kozi ya Grassroot jambo ambalo hapo awali ilikua ni nadra kutokea, hivyo amewataka washiriki hao kwenda kuwa mabalozi na kuwahamasisha wanawake wengine kuingia katika fani ya ukocha ambayo kwa hivi sasa imekua ikitoa ajira kwa vijana wengi bila kujali jinsia zao.

Naye mkufunzi wa kozi hiyo Raymond Gweba aliupongeza uongozi wa TFF kwa muendelezo mzuri wa kozi za grassroots ambazo zimekua zikitolewa katika mikoa mbalimbali, lengo ikiwa ni kuhakikisha tunakuwa na waalimu wa kutosha katika shule za msingi na vituo mbalimbali ili kuwafundisha watoto namna ya kucheza na kuvutiwa na mpira wa miguu.

Mafunzo ya grassroot yatatolewa kwa siku tano yakijumuisha mada 15 za malezi na makuzi ya watoto kwa mfumo wa nadharia na vitendo.