TFF yaendesha kozi ya kwanza ya VAR kwa waamuzi

Shirikisho la mpira wa miguu Tanzania (TFF) limeendesha semina ya kwanza ya teknolojia ya video inayomsaidia mwamuzi kufanya maamuzi kiwanjani (VAR- Video Assistant Referee) inayofanyika katika ukumbi wa King Jada, Dar es salaam.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa semina hiyo Mkurugenzi wa mashindano wa TFF Salum Madadi alisema, Mpira wa miguu kwa sasa umebadilika na teknolojia pia imekua kwa haraka hivyo ni vyema waamuzi wakazingatia mafunzo hayo yanayotolewa ili waweze kufanya kazi kwa weledi na kuendana na Kasi ya mabadiliko ya teknolojia.

“Mkizingatia mafunzo haya na mengine yatakayofuata nina imani Tanzania itakuwa ni miongoni mwa nchi zenye waamuzi bora barani Afrika. Badilisheni mtazamo wa watu wa kuona Tanzania haina waamuzi bora  kwa kuongeza umakini katika maamuzi mnayoyatoa uwanjani. Alisema Madadi.

Naye mkufunzi wa  FIFA na CAF Janny Sikazwe aliipongeza TFF kwa  kuona muhimu wa kuendesha mafunzo ya VAR kwasababu ni moja ya kigezo muhimu kwa waamuzi ili waweze kuchezesha mashindano makubwa ya Dunia, Afrika na mengineyo.

Mafunzo hayo yamejumuisha waamuzi 30 kutoka Tanzania Bara na visiwani na yatafanyika kwa muda wa siku tano.