TFF Yagawa mipira Elfu moja kwa mikoa ya Tanzania

Shirikisho la mpira wa miguu Tanzania (TFF) limegawa mipira Elfu moja kwa mikoa yote ya Tanzania  kwa ajili ya mradi maalum wa ‘Football For Schools’ unaofadhiliwa na Shirikisho la mpira wa miguu duniani ‘FIFA’.

Lengo kuu  la mradi wa ‘Football For Schools’ ni kuhakikisha  vijana wa kike na kiume wanapata nafasi  ya kucheza mpira wakiwa na vifaa sahihi hususani ni mipira ya kuchezea ili kutengeneza taifa linalojitoshelaza na kupungza idadi ya wachezaji kutoka nje.

Akizungumza wakati wa hafla ya ugawaji wa mipira hiyo iliyofanyika katika Ofisi za TFF Kigamboni, Dar es salam, Rais wa TFF Wallace Karia alisema “ programu hii ni kwajili ya mikoa ya Tanzania Bara na visiwani lakini kwa hatua za mwanzo ni mikoa 14 ndio itakayojumuishwa katika mradi huu”.

“Tanzania imebahatika kuwa miongoni mwa nchi zilizochaguliwa kuwa sehemu ya mradi huu ambao tuna imani utaleta mabadiliko makubwa katika tasnia ya michezo hivyo niwaombe wawakilishi wote wa mikoa (FA) na waalimu wa michezo mkasimamie vizuri vifaa vinavyotolewa na kuhakikisha vinawafikia walengwa ili taifa la Tanzania liweze kupiga  hatua katika tasnia ya michezo” alisema Karia.

Akizungumza kwa niaba ya wenyeviti wa mikoa, Mwenyekiti wa mkoa wa Tanga Martin Kibua aliipongeza TFF kwa kugawa mipira kwa mikoa  mbalimbali  na kusema kwamba mipira hiyo itatatua changamoto kubwa ya ukosefu wa mipira sahihi ya watoto kuchezea  mashuleni.

Mbali na Rais wa TFF Wallace Karia, hafla hiyo ilihudhuriwa na  Rais wa ZFF Dkt. Suleiman Jabir,  Makamu wa kwanza wa Rais  wa TFF Athuman Nyamlani, Makamu wa pili wa Rais wa TFF Steven Mnguto , Mwenyekiti wa Bodi ya wadhamini ya TFF Mohammed Abdulaziz, Katibu Mkuu wa TFF Kidao Wilfred, Mkurugenzi wa Ufundi wa TFF Oscar Mirambo , wenyeviti wa mikoa mbalimbali yaTanzania (FA) pamoja na waalimu wa michezo kutoka shule mbalimbali.