TFF Yaipiga Msasa Simba SC Masuala ya Uadilifu
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania TFF kupitia Mkurugenzi wa ukaguzi na udhibiti Hassan Njama limeendesha mafunzo ya Uadilifu Novemba 24, 2024 kwa klabu ya soka ya Simba SC ikilenga wachezaji, benchi la ufundi na uongozi kwa ujumla.
Mafunzo hayo ambayo ni muongozo kutoka Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) yameelekezwa moja Kwa moja kwenye timu zilizopata nafasi ya kushiriki mashindano ya Afrika (Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho) hususani katika hatua ya makundi.
Akizungumza baada ya mafunzo hayo Mkurugenzi wa ukaguzi na udhibiti TFF Hassan Njama alisema pamoja na kupitia maswala mbalimbali yanayohusu Uadilifu kwenye mpira wa miguu lakini pia walijadili juu ya kuoiga vita upangaji wa matokeo, matumizi ya dawa za kuongeza nguvu michezoni na kupambana na rushwa.
Alisema wamejadili kwa kina Uadilifu na vitu vyote vinavyohusiana na Uadilifu michezoni, lakini pia baada ya majadiliano ya kupinga vitendo visivyokuwa vya kiadilifu waliopata fursa ya kugawa fomu za makubaliano kwa wachezaji, benchi la ufundi na viongozi wengine kuthibirisha kwamba hawatojihusisha na maswala au matendo yoyote yasiyokuwa ya kiadilifu michezoni.
Aidha alieleza kuwa baada ya kila mmoja kumaliza kujaza fomu hizo pamoja na kuweka sahihi zao watapaswa pia kuambatanisha picha zao, huku akiweka bayana kuwa alikuwa na wakati mzuri siku zote alipokuwa anatoka mafunzo hayo.
Ikumbukwe TFF kupitia Mkurugenzi huyo na Maofisa wengine walikuwa na siku mbili za mafunzo hayo Kwa timu hizo zinazoshiriki mashindano ya CAF ambapo ilianza na klabu ya soka ya Young Africans Novemba 23,2024 Kisha kumalizia na Simba SC Novemba 24, 2024.