TFF Yasaini Mkataba wa Miaka Mitano na UNFPA

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania TFF limesaini mkataba wa mpango kazi wa miaka mitano na shirika la UNFPA (United Nations Population Fund) Novemba 16, 2022 katika hoteli ya Hyatt Regency Jijini Dar es Salaam.

Lengo kuu la makubaliano hayo ni kurudisha kwa jamii na kuifanya Tanzania iwe sehemu salama kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu ikilenga kutokomeza vifo vinavyozuilika wakati wa uzazi, kutokomeza maambukizi mapya ya virusi vya ukimwi, kuzuia ndoa za utotoni na kuhakikisha malengo ya kila kijana yanafanikiwa.

Akizungumza katika hafla hiyo ya utiaji saini Rais wa TFF Wallace Karia alisema ni faraja kubwa kwa TFF kuendelea kupata wadau mbalimbali katika kufanikisha kampeni zenye lengo la kuikomboa jamii kutoka katika vitendo vya unyanyasaji na vifo kwa wanawake wakati wa kujifungua.

“Hii si mara ya Kwanza kwa TFF kufanya kampeni zinazoigusa jamii moja kwa kwa moja, tumekuwa na kampeni nyingi ikiwemo ‘Nyumba ni choo’ ‘Sensa ya watu na makazi 2022’ na nyinginezo. Hivyo kwa kushirikiana na UNFPA tutahakikisha tunaifikia jamii kwa kuwaelimisha madhara yatokanayo na ndoa za utotoni, lakini pia uzazi wa mpango na faida zake tukizielekeza kampeni hizo katika mashindano yetu mbalimbali kuanzia ligi ya vijana, ngao ya jamii na hata mitandao ya kijamii ambayo tunaamini inawafikia watu wengi” alisema Karia.

Naye mkurugenzi mkazi wa UNFPA Mr. Mark Bryan Schreiber aliushukuru uongozi wa TFF kwa makubaliano waliyofikia na kusema kwamba TFF ni sehemu Sahihi ambayo itaifikia jamii kwa urahisi kupitia mchezo wa mpira wa miguu ambao unapendwa na watu wengi duniani. Kwani anaamini kupitia kampeni mbalimbali zitakazofanywa na wachezaji pamoja na wadau mbalimbali wa TFF zitaleta mabadiliko chanya kwa jamii.