Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) limethibitisha Tanzania kuwa na timu 4 katika mashindano ya Kimataifa kwa msimu wa 2019/2020.

Timu 2 zitashiriki katika Ligi ya Mabingwa na timu 2 nyingine zitashiriki Kombe la Shirikisho.

Nafasi hiyo kwa Tanzania imekuja baada ya kuwa katika nafasi 12 bora kwenye viwango vya ubora vya CAF.

Kwa mujibu wa Kanuni za Ligi Kuu zilizofanyiwa marekebisho na Kamati ya Utendaji baada ya kupatikana nafasi nne (4) timu za Tanzania zitakazowakilisha kwenye mashindano hayo ni Simba na Young Africans Ligi ya Mabingwa (CAF CL),Azam FC na KMC Kombe la Shirikisho (CAF CC).

KMC atawakilisha Kombe la Shirikisho kwa mujibu wa Kanuni hiyo ambayo inatamka kama timu iliyomaliza nafasi ya 3 itakua ndio bingwa wa Kombe la FA basi mshindi wa 4 anapata nafasi ya kucheza Kombe la Shirikisho kwasababu bingwa wa FA anaiwakilisha nchi kwenye mashindano hayo.

Tayari CAF imefungua dirisha kwa Mashirikisho kusajili timu kupitia mtandao wa CMS.

Mwisho wa usajili ni Juni 30,2019 ambapo TFF inatakiwa iwe imesajili timu zitakazoshiriki kwenye mashindano ya Kimataifa msimu wa 2019/2020.

Rais wa TFF Wallace Karia amezitaka klabu zilizopat nafasi kusajili kwa umakini na kujiandaa kwa Mashindano ya CAF ili kutopoteza nafasi ya kuingiza timu nne katika mashindano ya CAF