Timu ya Taifa ya Soka la Ufukweni Kujipanga Kwa BAFCON

Timu ya Taifa ya Soka la Ufukweni iliyokuwa ikishiriki mashindano ya COSAFA Durban Afrika Kusini imehamishia nguvu na akili kwenye mashindano ya BAFCON.

Timu hiyo ya Taifa ilicheza na kupoteza mechi zake zote za hatua ya makundi imeondoshwa rasmi kwenye mashindano hayo ya COSAFA baadaya ya kupoteza kwenye mchezo wake wa mwisho Machi 20, 2024 Kwa magoli 2-1 dhidi ya Morocco.

Akizungumza baada ya mchezo huo kocha mkuu Boniface Pawasa alisema mashindano hayo yamekuwa ni somo Kwa timu hasa wachezaji, lakini pia benchi la ufundi limeweza kujuwa uwezo wa kila mchezaji binafsi na timu Kwa ujumla.

“Tuna maingizo ya wachezaji wapya 10 hivyo kupitia mechi hizi tumepata kufahamu ubora na mapungufu Kwa kila mchezaji na timu Kwa ujumla. Tunachukulia haya ni maandalizi ya kuyaendea mashindano ya BAFCON yanayo tarajia kuanza maandali yake mwishoni mwa mwezi wa Aprili kabla ya kufanyika rasmi Kwa mashindano hayo mnamo mwezi Novemba mwaka huu” alisema Pawasa.

Kwa upande wa nahodha Jaruph Juma akizungumza baada ya mchezo Kwa niaba ya wachezaji wengine alisema licha ya kupoteza kwenye mchezo huo na mingine wanaimani wamepata uzoefu mkubwa, sambamba na kupata muunganiko wa kikosi chao.

“Haturidhishwi na matokeo tuliyoyapata lakini tunaridhishwa na maendeleo ya timu na muunganiko uliopo kati yetu wachezaji wenye uzoefu na hata maingizo mapya. Faida kubwa tuliyopata kwenye mashindano haya ni muendelezo mzuri wa kuyaendea mashindano makubwa ya BAFCON” alisema Jaruph.

Ikumbukwe kwenye mashindano ya COSAFA timu ya Taifa ya Soka la Ufukweni ilikuwa kundi ‘B’ pamoja na timu za Angola, Msumbiji na Morocco.