TANZANIA imeendelea kufanya vibaya katika fainali za soka la ufukweni za Mataifa ya Afrika (BSAFCON) baada ya kufungwa mabao 12-2 na mabingwa watetezi Senegal katika mchezo uliochezwa Sharm El Sheikh, Misri jana. Huu ni mchezo wa pili ikicheza na kufungwa baada ya juzi kufungwa mabao 5-2 na Libya na kesho inamaliza mchezo wa mwisho hatua ya makundi kwa kucheza na Nigeria.

Tanzania katika robo ya kwanza ilifungwa mabao 5-0, robo ya pili ikazinduka na kufunga mabao mawili yaliyowekwa kimiani na Jumaa na Yahaya Tumbo baada ya kipa Juma Kaseja kuingia kuchukua nafasi ya Ibrahim Abdallah na Nigeria ikaongeza mabao matano na kumaliza robo ya pili kwa mabao 10-2.

Robo ya tatu waliwabana wapinzani wao na kufanikiwa kupunguza idadi ya mabao kwani walifunga mabao mawili tu na kufanya mchezo kumalizika kwa mabao 12-2.

Kwa sasa Senegal inaongoza kundi B baada ya kushinda michezo yote miwili kwani juzi iliifunga Nigeria 6-4 ikifuatiwa na Nigeria ambayo jana iliifunga Libya kwa mabao 6-3 na Libya inashika nafasi ya tatu baada ya juzi kuifunga Tanzania 5-2.

Kundi A Madagascar jana iliifunga Ivory Coast mabao 3-4 hivyo Madagascar na Misri ambayo juzi iliifunga Morocco kwa mabao 6-1 Morocco zinaongoza. Tanzania leo itacheza na Nigeria na katika kundi A, Morroco itacheza na Ivory Coast na Madagascar itacheza na Misri na kesho Senegal itacheza na Libya, Morocco itaivaa Madagascar na Misri watamaliza na Ivory Coast.

Nusu fainali zitaanza kuchezwa Desemba 12 na fainali zitachezwa Desemba 14 na washindi wawili wa juu watakata tiketi ya kwenda kushiriki fainali za Kombe la Dunia mwakani nchini Paraguay. Fainali zijazo zitakazochezwa mwaka 2020 zitafanyika Uganda.