Dar es Salaam. Timu ya Taifa ya Tanzania ya soka la ufukweni, inatarajiwa kuingia kambini Ijumaa hii kujiandaa kwa michuano ya kufuzu kwa fainali za Afrika.
Hayo yalibainishwa jana na Meneja wa timu hiyo Deo Lucas, alipozungumza na Mwananchi jijini Dar es Salaam kuelezea maandalizi yao kuelekea mechi za kufuzu fainali za Afrika.
Deo alisema kikosi hicho kinachonolewa na mlinzi wa zamani wa Simba, Boniface Pawasa, kitaweka kambi kwenye hosteli za Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
“Kuhusu maandalizi tunatarajia kuingia kambini Ijumaa hii kuanza maandalizi ya mchezo wetu dhidi ya Afrika Kusini maana zimebakia kama wiki tatu hivi,” alisema Lucas.
Alisema mchezo wa kwanza baina ya Tanzania na Afrika Kusini unatarajiwa kuchezwa hapa nchini Septemba 9 na marudiano yatafanyika kati ya Septemba 21 na 23 nchini Afrika Kusini.
Lucas alisema kuwa mshindi wa jumla baina yao atajikatia tiketi ya kucheza fainali hizo zitakazofanyika nchini Misri Desemba mwaka huu.