Timu ya Taifa ya U20 Kurejea Nyumbani
Timu ya Taifa ya vijna wenye umri chini ya miaka 20 (U20) inatarajia kurejea nchini Tanzania ikitokea Sudani ilikokwenda kushiriki mashindano ya Baraza la Mpira wa Miguu la Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) ya kuwania teketi ya kushiriki michuano ya AFCON itakayofanyika nchini Misri 2023.
Timu hiyo inatarajiwa kuwasili Novemba 8, 2022 baada ya kupambana kiume kuisaka tiketi ya safari ya kuelekea Michuano hiyo ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) hapo mwakani kukutana na vizingiti vilivyosababisha juhudi za asakari hao vijana wa Kitanzania kushindwa kuzaa matunda na kufikia malengo yao ya kuwawakilisha Watanzania kwenye michuano hiyo mikubwa Afrika hapo mwakani.
Akizungumza baada ya michezo hiyo miwili, kocha wa timu hiyo ya U20 ya Tanzania Zuberi Katwila alisema vijana wake wamepambana kiume lakini haikuwa riziki kwani kila juhudi za kuhakikisha timu inapata matokeo chanya zilifanyika bado hazikuweza kuzaa matunda.
Aidha, kocha Katwila aliongeza kwa kusema kuwa kutolewa katika michuano hiyo kunatoa fursa nyingine ya kujifundisha mbinu nyingi za ziada ili kuweza kufanya vizuri zaidi katika michuano mingine ya aina hiyo mara inapotokea akisema kuwa kushiriki mara kwa mara kunawapatia vijana uzoefu na kujiamini Zaidi na hivyo kuweza kufanya vyema.
Vijana hao wa U20 walitoka sare ya bao 2-2 dhidi ya Ethiopia baada ya kupoteza mchezo wake wa kwanza kwa bao 2-0 dhidi ya Uganda na hivyo kumaliza ikiwa katika nafasi ya tatu katika kundi “B” ambapo timu zilizofanikiwa kusonga mbele kwenye hatua ya nusu fainali ni Ethiopia na Uganda.