Timu ya Taifa ya Wanawake U20 “Tanzanite” imefanikiwa kukata tiketi ya kucheza nusu Fainali ya Mashindano ya COSAFA yanayoendelea Port Elizabeth,Afrika Kusini.
Baada ya ushindi wake wa mabao 8-0 dhidi ya Eswatini,Tanzania imefanikiwa kutinga hatua hiyo ya nusu fainali kutoka Kundi B sambamba na Zambia wote wakiwa na alama 6.
Tanzania inaongoza Kundi B ikiwa na tofauti nzuri ya magoli ya kufunga na kufungwa ambapo imefunga 10 haijaruhusu nyavu zake kuguswa wakati Zambia wamefunga mabao 8 na kuruhusu nyavu zao kutikiswa mara moja.
Katika Kundi A Afrika Kusini tayari wamefuzu wakisubiri kuungana na Zimbabwe ama Namibia wote wakiwa na alama 3.
Mpaka sasa katika mashindano hayo Tanzania ndio timu iliyopata ushindi mkubwa zaidi wa mabao 8-0 na ndio timu iliyopata mabao mengi zaidi katika mchezo mmoja.
Aidha imefanikiwa kutoa mchezaji Bora wa mechi mara mbili mfululizo kupitia kwa mchezaji wake Diana Msemwa wakati Aisha Masaka akiondoka na mpira baada ya kutupia mabao 3 katika mchezo mmoja.
Mchezo wa kukamilisha hatua ya Makundi Tanzania na Zambia utachezwa Agosti 6,2019.