TMA,Kasulu United Kuzifuata TRA na Stand United Nusu Fainali

Mwendelezo wa michezo ya kundi B katika mashindano ya Fainali za Ligi ya Mabingwa wa Mikoa yanayo fanyika mkoani Kilimanjaro, mechi mbili zilizo pigwa Machi 30, 2022 katika uwanja wa Limpopo TPC zimemalizika kwa timu ya TMA kutokea Arusha na Kasulu United ya Kigoma zikipata nafasi ya kusonga mbele kwenye hatua ya nusu Fainali.

Mechi ya mapema kupigwa katika dimba hilo ilimalizika kwa TMA kupata ushindi wa magoli 2-0 dhidi ya Silent Ocean ya Dar es salaam ambayo imemaliza mashindano hayo ikiwa na alama 3 pekee  walizo zipata kwenye ushindi wa mechi yao ya kwanza kwenye hatua hiyo  dhidi ya City Gold.

Mchezo wa mwisho uliochezwa majira ya saa 10:00 jioni ulimalizika kwa Kasulu United kupata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya City Gold, timu ambayo pia inamaliza mashindano huku ikiwa na kadi nyekundu kwa mchezaji wake mmoja kama ilivyokuwa kwa timu ya kundi A Nzega United ambayo pia imetolewa katika hatua hiyo.

akizungumza mara baada ya mchezo kumalizika kocha wa Kasulu United Mohamed Seleman alisema kuwa kushinda katika mchezo huo zilikuwa ni mbinu pamoja na ujanja wa wachezaji wake kutumia nafasi walizo zipata, na kwamba malengo yao ni kufika mpaka hatua ya fainali hivyo watakwenda kujipanga ili kupambana zaidi.

Hatua ya makundi (Nane Bora) imemalizika kwenye Fainali za RCL kwa jumla ya timu nne kutoka kundi A na B kufuzu  katika hatua ya nusu fainali, huku timu nyingine zikifungasha virago kujipanga kwa msimu mwingine. Mechi za nusu fainali zinatarajiwa kuchezwa Aprili 2, 2022 kwenye uwanja wa Limpopo TPC Kilimanjaro.