Tumejitahidi Kudhibiti Wapinzani Wasipate Bao la Ugenini

Kauli ya Kocha mkuu wa Timu ya Taifa ya wasichana chini ya miaka 20 (U20) Tanzanite Bakari Shime mara baada ya kupata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya timu ya Taifa ya Ethiopia katika mchezo wa awali katika raundi ya nne mashindano ya kutafuta nafasi ya kufuzu kushiriki kombe la Dunia huko nchini Costa Rica mwaka huu.

Mchezo huo uliochezwa katika dimba la Amani uliopo visiwani Zanzibar Januari 23,2022 majira ya sa 10:00 jioni ulimalizika kwa Tanzanite kupata bao 1 la pekee lililofungwa na mchezaji Christer Bahera aliyepiga mpira wa kufa dakika ya 64 ya mchezo na kulenga moja kwa moja kwenye lango la timu ya Ethiopia.

Kocha Bakari Shime alisema kuwa mechi haikuwa rahisi, na kwamba licha ya wao kutengeneza nafasi nyingi katika vipindi tofauti walifanikiwa kuitumia vyema nafasi moja pekee na kupata bao la ushindi. Huku akitaja majeruhi ya Aisha Masaka, Clara Luvanga na Emiliana yalivyoweza kudhoofisha timu baada ya wachezaji hao kucheza chini ya viwango vyao.

Hata hivyo amekipongeza kikosi chake kwa kucheza vizuri hasa katika kipindi cha pili, sambamba na kuwapongeza mashabiki waliofika uwanjani kushuhudia mchezo huo kwa sapoti na hamasa waliyoweza kuitoa kwa timu pale ilipoonekana kuwa chini kwa kipindi chote cha mchezo.

“Tumeweza kufanikisha lengo la kuwadhibiti wapinzani wetu wasipate bao la ugenini, hivyo tunajipanga kwenda katika mchezo wa marudiano huku tukiwa na mtaji wa bao moja na tutaanzia hapo kwenda mbele.”Maneno ya kocha Shime.

Hatua hiyo ya mashindano inahusisha timu takribani 8, ambapo zinatafutwa timu 4 pekee ambazo zitakwenda katika hatua inayofuata kisha timu mbili ambazo ndio lengo hasa zitakazo kwenda kushiriki kombe la Dunia kuwakilisha timu za bara la Afrika. Tanzanite itakwenda Karatu kwaajili ya kukita kambi yake ikijiwinda kuelekea katika mchezo wa marudiano dhidi ya Ethiopia unaotarajiwa kuchezwa mapema mwezi Februari, 2022.