Twiga Stars Kamili Kubakisha Alama Tatu Nyumbani

Timu ya Taifa ya wanawake “Twiga Stars” iliyokwenye orodha ya timu nane Afrika zilizo salia katika kusaka tiketi ya kufuzu michuano ya Olimpiki, Februari 23, 2024 itajitupa cha kusaka ushindi dhidi ya Afrika Kusini mchezo utakaochezwa uwanja wa Azam Complex Chamazi, jijini Dar es Salaam, saa 1:00 usiku.

Kuelekea mchezo huo Kocha Mkuu wa Twiga Stars Bakari Shime alisema kwa asilimia kubwa maandalizi ya mchezo huo yamekamilika hivyo kikosi kinasubiri muda ufike kwani amesema mechi hiyo ni kubwa kwa kila mchezaji kuweka historia kwa mara nyingine.

Aidha alisema katika mashindano hayo kwa Afrika zimebaki nchini nane pekee ikiwemo Tanzania, huku akikumbushia kwa  mara ya mwisho walipoifunga timu ya Taifa ya  Botswana rekodi inayothibitisha Twiga Stars kushinda mechi zake zote za hivi karibuni.

“Nawapongeza wachezaji wangu kupambana hadi kufikia hatua hii ya mwisho kutafuta nafasi ya kufuzu Olimpiki, tunaenda kucheza mchezo mkubwa kulingana na wapinzani tunaokutana nao.Tukumbuke tunacheza na mabingwa wa Afrika, hatuwezi kuwa wakubwa hadi tucheze na timu kubwa, tunahitaji kucheza Olimpiki hivyo hatuwezi kukwepa kukutana na timu kubwa kama Afrika Kusini,” alisema kocha Shime

Akizungumza kwa niaba ya wachezaji, Oppa Clement alisema mchezo huo ni mkubwa na kwamba wachezaji wako tayari kwa ajili ya kupambana kutafuta matokeo mazuri.Huku akisisitiza hawana presha yoyote kuelekea mchezo huo.

“Tumejipanga vizuri na tuko tayari kwa mchezo wetu dhidi ya Afrika Kusini kutafuta nafasi ya kufuzu Olimpiki, tuko vizuri na tunasubiri muda wa kwenda uwanjani kikubwa tunaomba watanzania kujitokeza kwa wingi uwanjani kusapoti timu,” alisema Oppa.

Kwa upande wa kocha wa timu ya Taifa ya Afrika Kusini,  Desiree  Ellis alisema  maandalizi yameenda vizuri ni mchezo muhumu kuhakikisha wanafanikiwa kupata ushindi dhidi ya Tanzania.

“Tumefanya maandalizi na tupo tayari kutafuata matokeo mazuri, tunafahamu hautakuwa mchezo rahisi lakini tumekuja kutafuta matokeo chanya,” alisema Desiree.

Naye mchezaji wa Afrika Kusini  Thembi Kgatlana kwa niaba ya wachezji wengine alisema kuwa wamekuja kutafuta matokeo mazuri kwa ajili ya kufuzu Olimpiki hivyo lazima wapambane katika mchezo wa huo.

Ikumbukwe Twiga Stars ikifanikiwa kufuzu katika hatua hiyo itakuwa imesalia hatua moja pekee ili kujihakikishia tiketi ya michuano hiyo ya Olimpiki.