Twiga Stars Mabingwa COSAFA 2021

Timu ya Taifa ya Tanzania Twiga Stars imefanikiwa kubadili rekodi ya timu ya Taifa ya Afrika Kusini waliokuwa mabingwa wa mashindano ya COSAFA Women’s Championship mara saba mfululizo baada ya kupata ushindi wa bao 1-0 kwenye mchezo wao wa fainali dhidi ya Malawi.

Mchezo huo uliowatawaza Twiga Stars kuwa mabingwa wa mashindano msimu huu ulichezwa majira ya saa 9:00 Alasiri Afrika Kusini; sawa na saa 10:00 jioni kwa saa za Afrika ya Mashariki, ulimalizika kwa Twiga timu hiyo ya Tanzania kuendelea na rekodi yake iliyoanza nayo tangu mchezo wake wa kwanza ya kuchukua tuzo ya mchezaji bora.

Mchezo huo wa fainali kwa kipindi kirefu ulionekana kuwa mgumu kwa upande wa timu zote hivyo kupelekea uhaba wa magoli. Licha ya ugumu wa mchezo huo bado timu ya Taifa ya Tanzania ‘Twiga Sars’ ilipambana na hatimaye kufanikiwa kupata bao la kuongoza mnamo dakika ya 63 likipachikwa kambani na mchezaji Enekia Kasonga bao lililosalia mpaka kuamlizika kwa fainali iliyowapatia ubingwa Watanzania.

Mchezaji aliyechukua tuzo ya mchezaji bora wa mechi ni nahodha wa kikosi cha Twiga, Amina Bilali ambaye pia ndiye aliyechukua tuzo ya mchezaji bora kwenye mchezo wa nusu fainali waliocheza na Zambia.

Ikumbukwe kuwa ni mwishoni tu mwa mwaka 2020 ndipo timu ya Taifa ya Wanawake U17 ndio ilikuwa bingwa wa mashindano hayo kwa umri huo, ambapo pia mwaka mmoja nyuma (2019) timu ya Taifa ya Tanzanite (U20) nao walichukua ubingwa kwenye mashindano kama hayo.

Mwaka huu Twiga Stars ikaalikwa na ikasema inakwenda kuhakikisha makosa yote ya huko nyuma wanayafanyia kazi huku lengo lao kubwa zaidi likiwa ni kubeba kombe na kurudi nalo nyumbani Tanzania, lengo ambalo bila shaka limetimia.

Kocha Mkuu wa Twiga Stars, Bakari Shime alisema kuwa amefurahi kwa ubingwa lakini kubwa zaidi ni mafunzo ambayo wameyapata kwenye mashindano hayo akiamini kupitia mechi walizozicheza kwao ni kipimo kikubwa katika kufikia malengo ya kuendelea kuijenga timu hiyo.

Aidha, alieleza kuwa kinachofuata kwao hivi sasa ni kuangalia katika mashindano yaliyo mbele yao ambayo ndiyo wamekuwa wakiyafanyia maandalizi ya muda mrefu ya (KUFUZU AFCON) ambapo itawabidi kupigania nafasi nne za kuwakilisha Afrika kwenye Kombe la Dunia mwaka 2023.

Twiga Stars sasa inajiandaa kurejea nchini Tanzania ili kujiweka sawa na mchezo uliombele yao ambapo watashuka dimbani Oktoba 20, 2021 dhidi ya Namibia, Twiga Stars akiwa ni mwenyeji wa mchezo huo kisha kurudiana mwezi huo tarehe 23, 2021.

Kikosi cha Twiga Stars kilichoanza ni; Janeth Simba (JZ 01), Julitha Singano (JZ 15), Anastazia Katunzi (JZ 02), Happynes Mwaipaja (JZ 19), Enekia Kasonga (JZ 17), Fatuma Suleiman (JZ 05), Janeth Christopher (JZ 12), Stumai Athuman (JZ 08), Amina Bilali (JZ 04), Opa Tukumbuke (JZ 18) na Mwanahamis Omary (JZ 07).

Wachezaji wa akiba; Zubeda Mgunda (JZ 20), Husna Mtunda (JZ 21), Mariam Juma (JZ 22), Clara Luvanga (JZ 14), Koku Kipanga (JZ 13), Mwamvua Haruna (JZ 09) na Eva Jackson (JZ 03).