Twiga Stars Yaanza Kibabe, Yawaduwaza Wazimbwe
Timu ya Taifa ya Tanzania ‘Twiga Stars’ imeanza vizuri kwenye mchezo wake wa kwanza wa mashindano ya COSAFA Women’s Champion yanayofanyika kwenye mji wa Port Elizabeth nchini Afrika Kusini ambako Septemba 29,2021 timu hiyo ilishuka dimbani na timu ya Zimbabwe.
Mchezo huo uliopigwa kwenye Uwanja wa Nelson Mandela Bay (NMB) majira ya saa 9:30 alasiri kwa saa za Afrika Kusini sawa na saa 10:30 kwa saa za Afrika Mashariki ulimalizika kwa Twiga Stars kuibuka na alama tatu muhimu za ushindi mnene wa mabao 3-0.
Mchezo huo ulioonekana kuwa mgumu kwa pande zote kutokana na hali ya hewa ( mvua na baridi kali) haikuwa rahisi kwa timu yoyote kuweza kupata mabao mapema, hivyo iliwachukua muda kwa kila mmoja kuweza kumsoma mwenzake na hatimaye kutengeneza nafasi za kupata matokeo.
Hata hivyo, Twiga Stars kwa upande wao dakika 45 za kwanza ziliwatosha kupata goli la kutangulia lililofungwa na Donisia Daniel Minja (JZ 06) Mnamo dakika ya 41, goli hilo lilisalia mpaka dakika 45 za kipindi cha kwanza zinakamilika.
Kipindi cha pili kilianza kwa kushambuliana zaidi ambapo Twiga Stars waliokuwa mbele kwa faida ya bao moja walionekana kuongeza kasi zaidi ya mashambulizi ambayo yalionekana kuwa na faida kwa timu baada ya Mwanahamisi Omary(JZ 07) ambaye ndiye aliibuka kuwa mchezaji bora wa mchezo alipoweza kuiandikia timu yake bao la pili kabla ya mchezaji Aisha Masaka (JZ 10) alietokea BENCHI alichukua nafasi ya Opa Clement Tukumbuke ( JZ 18) kupachika bao la tatu.
Baada ya kumalizika kwa mchezo huo kocha Mkuu wa Twiga Stras Bakari Shime alisema kuwa amefurahi kwa ushindi huo licha ya hali ya hewa iliyopelekea kufanya mchezo kuwa mgumu, amekipongeza kikosi chake kwa kujitahidi kupata matokeo muhimu kwenye mchezo huo.
Aidha, kocha aliushukuru uongozi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kwa sapoti pamoja Serikali ya Awamu ya Sita inayoongoza na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuweza kupambania timu hizo za wanawake ili ziweze kuwa bora zaidi.
Aliongeza na kusema hayo, sambamba na kuwaahidi kuwa timu itahakikisha wanafanya vile ambavyo TFF na Serikali wanatarajia kutoka kwao ikiwa pia ndio malengo ya timu hiyo ili waweze kushiriki kwenye mashindano ya AFCON tena kwa mafanikio makubwa.
Kikosi kilichoanza kwa Twiga Stars ni; Janeth Simba(01) GK, Anastazia Katunzi(2), Amina Bilali(04), Fatuma Suleiman(05), Donisia Daniel Minja(06), Mwanahamisi Omary Shurua(07), Stumai Athumani(08), Diana Lucas Msewa(11), Julitha Singano(15), Opa Tukumbuke Clement(18) na Happyness Mwaipaja(19). Wakati wachezaji wa akiba wakiwa ni; Eva Jackson(03), Mwamvua Haruna(09), Aisha Masaka(10), Janeth Christopher Pangawene(12), Koku Kipanga(13), Enekia Kasonga(17), Zubeda Mgunda(20)GK na Husna Mtunda(21 GK).