Twiga Stars yafuzu WAFCON 2024

Timu ya Taifa ya wanawake ‘Twiga Stars’ imefanikiwa kufuzu kushiriki Fainali za Kombe la Mataifa Afrika kwa wanawake (WAFCON) zitakazofanyika mwakani nchini Morocco baada ya kupata ushindi wa jumla ya magoli 3-2 dhidi ya timu ya Togo.

Licha ya kupoteza katika mchezo wa mkondo wa pili  wa kufuzu WAFCON dhidi ya Togo kwa goli 2-0 katika uwanja wa Stade de Kegue, Togo, Twiga stars’ ilionyesha ushindani na ukomavu wa hali ya juu katika mchezo huo.

Akizungumza mara baada ya mchezo kumalizika Kocha Mkuu wa ‘Twiga Stars’ Bakari Shime alisema, kiujumla mchezo ulikua mgumu sana tulikua na nafasi kubwa  ya kushinda hasa katika kipindi cha kwanza kwasababu tulitengeneza nafasi nyingi za kufunga  lakini kwa bahati mbaya washambuliaji wetu walikosa umakini na walishindwa kutumia nafasi hizo vizuri.

“Niwapongeze wachezaji wa ‘Twiga stars’ kwa kucheza vizuri na kuliheshimisha Taifa la Tanzania kwa kuwa miongoni mwa timu 12 zitakazocheza WAFCON 2024 nchini Morocco. Ni timu kubwa nyingi zilitamani kufuzu lakini zilishindwa hii ni nafasi ya ‘Twiga Stars’ kuonyesha ukubwa wake na kujipanga vizuri kwa ajili ya kushindana katika mashindano hayo na mengine ya kimataifa yaliyo mbele yetu”.  alisema Kocha Shime

Twiga Stars inakuwa timu pekee kutoka Ukanda wa CECAFA kufuzu kushiriki Fainali za Kombe la Mataifa Afrika kwa wanawake (WAFCON) baada ya timu ya Kenya (Harambee Starlets) kupoteza mbele ya Botswana kwa goli 1-0. Timu ya Burundi nayo imeshindwa kukata tiketi ya kufuzu WAFCON baada ya kupoteza mbele ya Algeria kwa goli 1-0.

Ni timu 12 ambazo zimefuzu WAFCON 2024 ambazo ni Tanzania,  Botswana, Zambia, Ghana, Senegal, Mali, South Africa, Tunisia, Algeria, DR Congo, Nigeria  pamoja na mwenyeji Morocco.