Twiga Stars yaichapa Botswana goli 2-0 Azam Complex

Timu ya Taifa ya Wanawake ‘Twiga Stars’ imeichapa timu ya Botswana goli 2-0 katika mchezo wa kufuzu kushiriki mashindano ya Olimpiki uliochezwa katika uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.

Mchezo huo wa raundi ya pili ulichezwa majira ya saa 10 kamili Jioni ambapo ‘Twiga stars’ walionyesha kuutawala mchezo katika dakika 45 za kipindi cha kwanza na  goli la mapema lilifungwa na Oppa Clement kwa Mikwaju wa Penati dakika ya 2 ya mchezo huku goli la  pili likifungwa na mchezaji Aisha Masaka katika dakika ya 85.

Akizungumza baada ya mchezo huo kumalizika Kocha Mkuu wa ‘Twiga stars’ Bakari Shime alisema, Timu imecheza vizuri licha ya changamoto kadhaa zilizojitokeza hasa katika eneo la kiungo lakini tunashukuru kwamba mabadiliko yaliyofanyika kipindi cha pili yalizaa matunda na tukafanikiwa kupata ushindi nyumbani.

“Tumeshinda nyumbani haijalishi ni magoli mangapi, tunakwenda ugenini na tuna amini tunaweza kupata matokeo kwa sababu tuna wachezaji wenye uwezo wa kutupa matokeo yatakayotupa tiketi ya Olimpiki mwaka 2024″ alisema Kocha Shime.

Naye kocha wa timu ya Botswana Mohambi Saulosi alisema ” tumepoteza ugenini kutokana na kukosa umakini mchezoni hivyo tukatoa nafasi kwa mpinzani wetu kutuadhibu na ndio mpira ulivyo, tunarudi nyumbani kujaribu kubadilisha matokeo” alisema Kocha Saulosi .

Twiga Stars itacheza mchezo wa marudiano dhidi ya Botswana Oktoba 31, 2023 nchini Botswana.