Twiga Stars Yarejea Dar na Kikombe cha COSAFA

Timu ya Taifa “Twiga Stars” imewasili katika uwanja wa Julius Kambarage Nyerere ikitokea Afrika Kusini ikiwa na Kombe ililolitwaa Oktoba 09, 2021 baada ya kuifunga Malawi bao 1-0 katika mchezo wa fainali ya COSAFA WOMEN’S CHAMPIONS 2021 uliopigwa nchini humo.

Timu iliwasili Dar es Salaam Oktoba 11, majira ya saa mbili usiku (02:00) na kupokelewa na viongozi wa Serikali, TFF na wafanyakazi pamoja na wadau walioambatana na mashabiki wa soka waliofika Uwanjani hapo kwa ajili ya kuwalaki mabingwa hao wa Kombe la COSAFA 2021.

Akitoa neno la pongezi kwa mabingwa hao, Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Hassan Abbas alikipongeza kikosi hicho cha Twiga kwa kupambana kwa hali na mali na kufanikiwa kurejea na Kombe hilo. Alisema kuwa yeye kwa niaba ya serikali anaona fahari kubwa kwa ushindi huo kwani umeendelea kuliletea sifa na heshma kubwa Taifa na kuonesha namna ambavyo nchi imejipanga kuhakikisha mafanikio hayo yanaendelea kupatikana.

Aidha, Katibu Mkuu huyo aliongeza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan imejipanga vilivyo kuhakikisha wachezaji wa michezo mbalimbali ikiwemo soka wanaendelea kufanya vizuri kila uchao kwa kuboresha zaidi mazingira ya michezo ambapo alisisitiza zaidi kuhusu soka la wanawake.

Zaidi ya hilo, alisema kwamba serikali tayari imekwisha kutenga fungu la fedha kwa ajili ya kusaidia masuala mbali mbali ya michezo ikiwemo mpira wa miguu nchini. Sambamba na hilo Dkt. Abbas alitoa mualiko rasmi kwa kuzikaribisha chaklula cha jioni timu zote; Tanzanite (U20) na Twiga Stars akisema kuwa serikali itakuwa na jambo lake jioni hiyo ya Oktoba 12, 2021.

Naye Mkurungezi wa Baraza la Michezo Tanzania (BMT) Omary Singo, aliongeza na kusema kuwa timu za wanawake zimekuwa zikifanya vizuri na kwamba wao kama moja ya wadau wa michezo wataendelea kushirikiana na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania ili kuhakikisha ushindi huo unaendelea kupatikana kati kila mashindano.

Kocha Mkuu wa Kikosi cha Twiga Stars akiwa Uwanjani hapo naye alisema kuwa anashukuru kufanikisha malengo waliyokuwa wamejiwekea ya kushinda na kutoa mchezaji bora katika kila mechi na kwamba mashindano hayo yamewapa uzoefu mkubwa kutokana na ubora wa timu walizokutana nazo kwenye michuano hiyo. Kocha Shime aliweka bayana kuwa sasa kilichobakia mbele yao ni kufanyia kazi makosa madogo madogo waliyoyabaini kutokana na michezo yote licha ya kufanikiwa kutwaa ubingwa huo.

Nahodha wa Twiga Stars Amina Bilal, alimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuwasaidia kurejea na kikombe huku akimmwagia sifa Kocha Mkuu Bakari Shime kwa kutoa maelekezo mazuri na hamasa kubwa kwa wachezaji,  akisema ushindi huo na uchezaji bora walioupata katika kila mechi na ule waa jumla alioupata yeye, unatokana na umoja waliokuwanao wao kama wachezaji pamoja na benchi la ufundi.

Mwanahamisi Omary naye ni mchezaji aliyefanikiwa kupata tuzo ya mchezaji bora wa mechi ya kwanza dhidi ya Zimbabwe, alifunguka akisema kuwa kitu kikubwa alichokipenda katika mashindano hayo kwa upande wa timu yao ni ubora uliooneshwa na kila mchezaji, ambapo alisema kwa kikosi hicho kilichoshiriki michuano hiyo endapo kitaendelea na umoja huo michezo yote kinaweza kufanya vizuri. Mchezaji huyo wa Kimataifa aliongeza kuwa, cha muhimu ni kila mchezaji kuendelea kujituma na kufuata maelekezo sahihi ya mwalimu na benchi zima la ufundi huku akitanabaisha kuwa kikosi chao kwa sasa hakitegemei umaarufu wa mchezaji mmoja; kwani kila mchezaji anaweza kufunga na kuchukua tuzo ya uchezaji bora kwenye mechi yeyote kama ilivyojidhihirisha kwenye mashindano hayo makubwa.

Wachezaji wengine waliofanikiwa kupata Tuzo za uchezaji bora wa mechi ni Fatuma Issa Suleiman Maonyo (Densa), na Stumai Abdallah Athuman (Kuchi 8) ambao wote walisema kuwa wamefurahi kurudi na ushindi na kwamba mashindano hayo yamewaongezea uzoefu mkubwa ambao utakuwa na faida kwenye michuano inayofuata hivi karibuni.

Mbali na viongozi waliotajwa awali, viongozi wengine waliofika Uwanjani hapo kwa ajili ya kuipokea Twiga Stars walikuwa ni Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi ambaye pia ni Makamu wa Pili wa Rais TFF Steven Mnguto, Mkurugenzi wa Ufundi wa TFF Oscar Mirambo, Mama Sephania Kabumba (Ofisa dawati la mpira wa miguu wa wanawake wa TFF pamoja na wafanyakazi wengine wakiwemo wanahabari wa TFF.