Twiga Stars yatinga hatua ya tatu kufuzu Olimpiki

Timu ya Taifa ya wanawake ‘Twiga Stars’ imefanikiwa kutinga hatua ya tatu ya kufuzu mashindano ya Olimpiki baada ya kuifunga Botswana goli 1-0 katika mchezo wa marudiano uliochezwa katika uwanja wa Taifa Gaborone, Botswana.

Goli pekee lililofungwa na mchezaji Aisha Masaka lilitosha kuwapeleka Twiga Stars katika hatua hiyo mara baada ya kuwafunga Botswana nyumbani goli 2-0 na ugenini goli 1-0 hivyo kujikusanyia jumla ya magoli 3-0. Katika hatua ya tatu Twiga Stars itakutana na timu ya Afrika Kusini.

Akizungumza baada ya mchezo huo kumalizika Kocha Mkuu wa Twiga Stars Bakari Shime alisema, ulikua mchezo mgumu kama ambavyo tulitarajia ambapo wapinzani wetu walionyesha ushindani wa hali ya juu na matumizi makubwa ya nguvu na kasi huku wakipiga mipira ya juu lakini tuliweza kuwadhibiti na kupata ushindi ugenini.

“Nawapongeza wachezaji kwa kazi nzuri waliyofanya, sasa tunakwenda kutathimini mapungufu yaliyojitokeza katika raundi mbili zilizomalizika ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kukabiliana na timu ya Afrika Kusini mwezi Februari katika raundi ya tatu” alisema Kocha Shime

Matokeo ya mechi nyingine za kufuzu Olimpiki zilizochezwa leo Oktoba 31,2023, Cameroon inasonga katika raundi ya tatu baada ya kuiondoa Uganda kwa jumla ya magoli 3-2 huku Morocco naye akimfunga Namibia goli 2-0 na hivyo kutinga raundi ya tatu kwa jumla ya magoli 4-0. Timu ya Nigeria ikatamba katika uwanja wa nyumbani kwa kuifunga Ethiopia goli 4-0 na kumaliza raundi ya pili ikiwa na jumla ya magoli 5-1.