Mchezo wa kirafiki kati ya timu ya U20 ya Tanzania na Sudani ulichezwa katika uwanja wa Uhuru Jijini Dar es Salaam huku timu ya Sudani ikijibu mapigo mara baada ya timu hiyo kupoteza mechi ya kwanza iliyopigwa Juma pili iliyopita (09/11/2020) kwenye uwanja wa Azam Complex uliopo Chamanzi Mbagala, pembezoni kidogo mwa Jiji hilo la biashara.

Katika mchezo huo uliopigwa majira ya saa 10:00 jioni ulikuwa wa kawaida kutokana na kikosi cha Tanzania kuingia uwanjani kikiwa na kumbukumbu ya kuwachapa Sudani jumla ya magoli mawili kwa moja na hivyo kuwafanya wajiamini zaidi tofauti na wapinzani wao ambao wao waliingia uwanjani wakiwa na kumbukumbu ya kupoteza mchezo wa awali.

Kama ilivyo ada kuwa mchezo wa mpira wa miguu huchezwa uwanjani na kwamba hakuna timu inyoweza kwenda uwanjani na matokeo yake; na mara nyingi mchezo huu huja na matokeo yasiyotarajiwa na wengi na hicho ndicho kilichowatokea wachezaji wa U20 wa  Tanzania ambapo wao waliingia uwanjani wakiwa na kumbukumbu ya kuwafunga Sudani katika mchezo wa awali 2-1.

Kipindi cha kwanza kilikuwa kizuri zaidi kwa Sudani kwani waliweza kuandika bao la kuongoza mnamo dakika ya 11 tu ya mchezo, bao lililofungwa na mchezaji jezi namba 02 aitwae Mustafa Nangi Hassan na kudumu kwa dakika zote 45 za kipindi cha awali na kuwafanya wenyeji Tanzania kwenda kwenye mapumziko wakiwa nyumba kwa bao moja kwa bila.

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi kiasi huku vijana wa Jumhuri Kihwelo wakitafuta bao la kusawazisha kwa udi na uvumba. Wakati wao wakisaka bao hilo la kusawazisha vijana wa Sudani walifanikiwa kuongeza bao la pili katika dakika ya 12 ya kipindi hicho, bao lililopachikwa wavuni na mchezaji mwenye jezi namba 08 Nagi Alamin na kuifanya timu ya  U20 ya Tanzania kuwa nyuma kwa bao 2-0.

Hata hivyo kabla kabumbu halijamalizika Tanzania nayo ikafanikiwa kupata bao kunako dakika ya 19 ya kipindi cha pili, bao lililofungwa na mchezaji jezi namba 11Teps Evas na kuufanya ubao wa matangazo kusoma 2-1 mpaka dakika 90 za mchezo huo zinamalizika.

Kocha wa timu ya Sudani Mounir Lehbab alisema kuwa amefurahi kwa wachezaji wake kuibuka na ushindi katika mchezo huo huku akishukuru kucheza mechi mbili za majiribio kwani zimemfanya kujua kikosi chake kina upungufu gani na kubaini maeneo yapi anapaswa kuboresha kabla ya kuingia katika michuano. Kocha huyo aliongeza kwa kukipongeza kikosi cha Tanzania kwa kusema kuwa ni kikosi bora na kina wachezaji wa kutosha kwani idadi kubwa ya wachezaji walioanza leo ni tofauti na wale walioanza katika mchezo wao wa kwanza.

Naye kocha Jamhuri Kihwelo alisema kuwa kikosi chake kimefungwa kutokana na makosa ya kimpira kama vile wenzeo walivyo poteza mchezo wa kwanza. Hivyo mashabiki wasiwe na shaka kuhusu uwezo wa kikosi chao cha U20 isipokuwa wakae tayari kupokea ushindi. Aidha kocha Kihwelo alisema kuwa sababu nyingine kuwa ni wachezaji wake kukosa muunganiko wa kutosha kutokana na kukaa pamoja kwa muda mfupi wa wiki 2 pekee. Hivyo kikosi hicho kinapaswa kuaminiwa na kupewa muda wa kutosha ili kiweze kutupa burudani inayoambatana na ushindi .

Wachezaji walioanza  katika kikosi cha Tanzania ni; Razak Shekimwel GK, David Kameta, Shabani Kingazi, Laurent Afreid, Samwel Jackson, Ally Msengi, Ally Abdi, Khelfun Salim, Kelvin John (C) na Nassoro Saadam; huku wachezaji walioanza kwa Sudani wao wakiwa ni; Omer Khamis GK, Mazin Bashir, Abdellatif Adam,Tawfif Yousif, Nangiel Adam,Aadam Mohmed,Mustafa Nagi Hassani, Wesam Haytham, AbdekarimAbdelrahmo, Nagi Alamin na Algozoli Hussein.

Katika mchezo wa kwanza uliopigwa Chamanzi timu ya U20 ya Tanzania iliibuka na bao 2-1 dhidi ya Sudani iliyopata matokeo kama hayo. Mechi hizi zilikuwa ni kwa ajili ya kujiweka katika hali nzuri kwa ajili ya michuano ya CECAFA inayotarajiwa kuanza kutimua vumbi mwishoni mwa mwezi Novemba, 2020 ambapo mashidano hayo yatafanyika katika Mkoa wa Arusha.