Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) katika kikao chake cha Oktoba 7, 2019 ilipitia mwenendo na matukio mbalimbali ya Ligi na kufanya uamuzi ufuatao;

Viwanja: Kamati imezuia baadhi ya viwanja kutumika kwa mechi za Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) na Ligi Daraja la Kwanza (FDL) kutokana na kuwa na upungufu katika maeneo mbalimbali ikiwemo la kuchezea (pitch) na uzio wa ndani unaotenganisha wachezaji na washabiki (fence).

Viwanja hivyo ni Kinesi Bull (Dar es Salaam), Bandari (Dar es Salaam), Jamhuri (Morogoro), Namfua (Singida), na Mkwakwani (Tanga).

Klabu ambazo timu zao zinatumia viwanja hivyo zimepewa nafasi ya kufanya marekebisho kipindi hiki ambacho Ligi zimepitisha mechi za kirafiki za FIFA au kuchagua viwanja mbadala vyenye sifa.

Vilevile klabu zimekumbushwa kuzingatia Kanuni ya 14(2), kwani baadhi yao zinapeleka viwanjani magari yenye kitanda badala ya gari la wagonjwa (ambulance).

Kanuni imezungumzia ambulance, na si gari lolote tu.

Wasimamizi wa mechi vituoni wanatakiwa kuhakikisha ambulance zinapokuwepo viwanjani kama ilivyoelekezwa kikanuni.

Kama huduma ya ambulance haitokuwepo wanatakiwa kuzuia mechi kuchezwa.

Ligi Kuu ya Vodacom

Mechi namba 19: Coastal Union 2 v KMC 0- Klabu ya KMC imetozwa faini ya sh. 1,000,000 (milioni moja) kutokana na timu yake kutoingia vyumbani wakati wa mapumziko katika mechi hiyo iliyochezwa Septemba 13, 2019 katika Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.

Adhabu hiyo ni kwa mujibu wa Kanuni ya 14(49) ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo.

Mechi namba 24: Alliance FC 1 v Biashara United 1- Klabu ya Alliance imetozwa faini ya jumla ya sh. 1,000,000 (milioni moja) kutokana na vurugu za washabiki wake pamoja na kufanya vitendo vinavyoashiria imani za ushirikina katika mechi hiyo iliyofanyika Septemba 20, 2019 Uwanja wa Nyamagana jijini Mwanza.

Nayo klabu ya Biashara United imetozwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) kwa kufanya vitendo vinavyoashiria imani ya ushirikiana wakati ikiingia uwanjani. Adhabu zote ni kwa mujibu wa Kanuni ya 43(1) ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti kwa Klabu.

Mechi namba 40: Kagera Sugar 0 v Simba 2- Mchezaji Zawadi Mauya wa Kagera Sugar amepewa Onyo kutokana na kitendo chake cha kumpiga mateke mchezaji wa Simba kwenye mechi hiyo iliyochezwa Septemba 26, 2019 katika Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.

Adhabu dhidi yake ni kwa mujibu wa Kanuni ya 14(49) ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo.

Naye Mwamuzi wa mchezo huo Emmanuel Mwandembwa amepewa Onyo kwa kumuonesha Mauya kadi ya njano badala ya nyekundu kwa kitendo chake ambacho kilikuwa cha makusudi na kujirudia.

Mechi namba 41: Singida United 0 v Alliance FC 2- Klabu ya Alliance imetozwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) kwa kumweka kwenye benchi la ufundi Meneja ambaye hakutambulishwa katika kikao cha maandalizi ya mechi (pre match meeting) wakati wa mechi hiyo iliyofanyika Septemba 28, 2019 Uwanja wa Namfua mjini Singida.

Adhabu hiyo imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 14(3) ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo.

Mechi namba 44: Lipuli FC 2 v Tanzania Prisons 2- Klabu ya Tanzania Prisons imetozwa faini ya sh. 3,000,000 (milioni tatu) kutokana na basi lililobeba wachezaji wa timu hiyo kuingia uwanjani kwa kutumia mlango usio rasmi katika mechi hiyo iliyofanyika Septemba 29, 2019 Uwanja wa Samora mjini Iringa. Adhabu imezingatia Kanuni ya 14(49) kuhusu Taratibu za Mchezo.

Ligi Daraja la Kwanza:

Mechi namba 8A: Boma FC 2 v Majimaji 0- Meneja wa timu ya Majimaji, Shaibu Ibrahim amefungiwa mechi tatu na kutozwa faini ya sh. 200,000 (laki mbili) kwa kutolewa katika benchi kwa kadi nyekundu baada ya kumtukana Mwamuzi katika mechi hiyo iliyochezwa Septemba 22, 2019 Uwanja wa Mwakangale uliopo Kyela, Mbeya.

Adhabu ni kwa mujibu wa Kanuni ya 42(20) ya Ligi Daraja la Kwanza kuhusu Udhibiti kwa Viongozi.

Mechi namba 10A: Dodoma FC 1 v Friends Rangers 0- Wachezaji Ahmed Abbas Iddy (Friends Rangers) na Mbwana Bakari (Dodoma FC) wamefungiwa mechi tatu na kutozwa faini ya sh. 300,000 (laki tatu) kila mmoja baada ya kutolewa nje kwa kadi nyekundu kwa kosa la kupigana katika mchezo huo uliofanyika Septemba 21, 2019 Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma.

Adhabu hiyo ni kwa mujibu wa Kanuni ya 38(3) ya Ligi Daraja la Kwanza kuhusu Udhibiti kwa Wachezaji.

Mechi namba 1B: Gwambina FC 3 v Arusha FC 0- Klabu ya Arusha imepewa Onyo kutokana na timu yake kuchelewa kuingia uwanjani kwa dakika 19.

Timu hiyo iliingia saa 9:19 badala ya saa 9:00 katika mechi hiyo iliyochezwa Septemba 14, 2019 kwenye Uwanja wa Gwambina mkoani Mwanza.

Vilevile Arusha FC imepewa Onyo Kali kutokana na wachezaji wake kuingia uwanja kwa kuruka uzio wa ndani badala ya kutumia mlango walioelekezwa.

Adhabu zote hizo ni kwa mujibu wa Kanuni ya 14(49) ya Ligi Daraja la Kwanza kuhusu Taratibu za Mchezo.

Mechi namba 2B: Geita Gold FC 2 v Mashujaa FC 2- Klabu ya Geita imepewa Onyo kutokana na timu yake kuchelewa kuingia uwanjani kwa dakika 20.

Timu hiyo iliingia saa 9:20 badala ya saa 9:00 katika mechi hiyo iliyochezwa Septemba 14, 2019 kwenye Uwanja wa Nyankumbu mjini Geita.

Adhabu ni kwa mujibu wa Kanuni ya 14(49) ya Ligi Daraja la Kwanza kuhusu Taratibu za Mchezo.

Kocha Msaidizi wa Mashujaa FC, Kajembe Abdallah amefungiwa mechi tatu na kutozwa faini ya sh. 300,000 (laki tatu) kwa kutolewa katika benchi kwa kadi nyekundu baada ya kumtukana Mwamuzi Msaidizi.

Adhabu ni kwa mujibu wa Kanuni ya 41(11) ya Ligi Daraja la Kwanza kuhusu Udhibiti kwa Makocha.

Mechi namba 9B: Gwambina FC 1 v Stand United 0– Kamishna Nestory Matiku amepewa Onyo kwa kutoa taarifa isiyojitosheleza ya mechi hiyo iliyochezwa Septemba 21, 2019 katika Uwanja wa Gwambina mkoani Mwanza.

Mechi namba 10B: Geita Gold FC 1 v Rhino Rangers 0- Meneja wa Rhino Rangers, Ali Rhumba amepelekwa Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) baada ya kumpiga Mwamuzi Msaidizi Omari Mataka na kumjeruhi chini ya jicho katika mechi hiyo iliyofanyika Septemba 21, 2019 kwenye Uwanja wa Nyankumbu mjini Geita.

Nao wachezaji wa Rhino Rangers (Simon Joseph Kiula juzi no. 5 na Julius Elias Masunga jezi no. 26) wanapelekwa Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kwa kuwarushia mawe waamuzi baada ya kumalizika mechi hiyo.

Polisi waliokuwa uwanjani walijitahidi kupambana na licha ya kupata upinzani kutoka kwa wanajeshi kadhaa waliombatana na Rhino Rangers.

Mechi namba 12B: Sahare All Stars 1 v Green Warriors 1- Kipa wa Green Warriors, Shabani Dihile amepewa Onyo Kali kwa kutoa shutuma dhidi ya waamuzi kuwa walichezesha kwa maelekezo ya viongozi mechi hiyo iliyochezwa Septemba 22, 2019 katika Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.

Adhabu ni kwa mujibu wa Kanuni ya 14(49) ya Ligi Daraja la Kwanza kuhusu Taratibu za Mchezo.

Mechi namba 13B: Stand United 3 v Green Warriors 2- Klabu ya Green Warriors imetozwa faini y ash. 200,000 (laki mbili) baada ya wachezaji wake kuingia uwanjani kwa kutumia mlango usio rasmi katika mchezo huo uliofanyika Septemba 27, 2019 Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga.

Adhabu ni kwa mujibu wa Kanuni ya 14(49) ya Ligi Daraja la Kwanza kuhusu Taratibu za Mchezo.

Mechi namba 17B: Pamba SC 1 v Geita Gold FC 2- Meneja wa Pamba SC, Jafari Juma amepelekwa Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) baada kwa kumpiga ngumi Mwamuzi, tukio lililosababisha askari polisi wamweke chini ya ulinzi katika mechi hiyo iliyofanyika Septemba 28, 2019 kwenye Uwanja wa Nyamagana jijini Mwanza.