Uganda Yaendeleza Ubabe kwa Stars

Timu ya Taifa ya Tanzania “Taifa Stars” imeshindwa kuonesha makali yake dhidi ya timu ya Taifa ya Uganda katika mchezo wa kirafika wa Kimataifa uliopigwa Disemba 09 katika uwanja wa Benjamin Mkapa baada ya kupoteza kwa bao 2-0; mchezo ukiwa ni maalum kwa ajili ya kusherehesha maadhimisho ya kumbukumbu za Uhuru wa Tanzania Bara.

Mchezo huo uliopigwa majiara ya saa 1:30 usiku kwa saa za Afrika Mashariki, ulikuwa na upinzani mkubwa hasa katika dakika 45 za kipindi cha kwanza ambapo hakuna timu iliyofanikiwa kupata bao lolote mpaka timu hizo zinakwenda kwenye mapumziko.

Baada ya kipindi cha kwanza kukamilika, kipindi cha pili kilianza huku kila timu ikifanya mabadiliko kadhaa kwa kutoa na kuingiza nguvu mpya jambo ambalo lilikuwa na faida zaidi kwa timu ya Uganda tofauti na ilivyokuwa kwa Stars.

Uganda walifanikiwa kupata bao la kuongoza kunako dakika 72 kipindi cha pili likipachikwa na mchezaji Avan Asaba huku Joseph Bright akipigilia msumari wa pili kunako dakika ya 90 ya mchezo huo, na kuufanya mchezo huo kutamatika kwa tofauti ya bao 2-0.

Kim Poulsen, kocha Mkuu wa kikosi cha ‘Taifa Stars’ baada ya mchezo huo alisema kuwa mchezo ulikuwa mzuri na kwamba amepoteza mechi hiyo lakini kikubwa alichokitaka ni kuona namna gani vijana chipukizi wanavyoweza kucheza mpira wakiwa wao wenyewe tu hususani pale inapotokea kukosekana kwa wachezaji wenye majina makubwa waliozoeleka kuonekana katika kila mechi za Taifa.

Aliongeza kuwa lengo na dhumnu la mchezo huo lilikuwa ni kujaribu kutizama vipaji vipya vilivyopo pamoja na kuiunga mkono Serikali katika kuadhimisha sherehe za Uhuru wa Tanzania Bara huku shabaha nyingine ikiwa ni kuimarisha uhusiano baina ya nchi husika na kuwapatia watanzania burudani. Hata hivyo, kocha huyo alidai kuwa kupoteza kwa mchezo huo kumetokana na wachezaji hao kukosa uzoefu wa kutosha, hali iliyopelekea kufanya makosa mengi yaliyosababisha wapinzani wao kuyatumia na kupata ushindi.

Kwa upande wake kocha wa Uganda “The Cranes” Sredojevic Micho yeye alisema kuwa anashukuru kwa ushindi alioupata, kwani ulikuwa ni mchezo mgumu na wenye ushindani licha ya kikosi chake kuibuka na matokeo mazuri. Aliendelea kusema kwamba timu yake ilitumia uzoefu na mbinu zaidi mara baada ya kuwasoma vyema Stars namna walivyokuwa wanacheza kisha kutumia udhaifu waliouonesha na kupata magoli hayo yaliyoipatia ushindi timu yake ya Uganda.

Mbali na hayo, kocha Micho aliongeza kwa kusema kuwa anawaheshimu walimu wote wa Stars akiona benchi hilo lina wachezaji nguli wa zamani kama akina Haroub Kanavaro, Shedrack Nsajigwa, Ivo Mapunda na kocha Mkuu Kim Poulsen kwa kuwandaa vyema wachezaji hao chipukizi ambao walikuwa wakicheza AFCON ya U20 pamoja na baadhi ya nyota wa kikosi chake.

Baadhi ya nyota waliounda kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania kwa ajili ya mchezo huo maalum wa kirafiki wa Kimataifa kwa upande wa Tanzania ni pamoja na; Metacha Mnata, Oscar Massai, Nickson Kibabage, Abdalmajid Mangalo, Abdulrazack Mohammed, Sospeter Bajana, Kelvin Nashon, Abdul Hamis Suleiman, Meshack Abraham, Vitalis Mayanga, na Reliant Lusajo. Wachezaji wa akiba walikuwa ni; Mussa Mbise, Sharoun Mandawa, Kelvin Kijiri, Tariq Simba, Hance Masoud, Nathan Chilambo, Rashid Juma, Hassan Nassor, Cleophas Mkanadala, Denis Nkane na Anuary Jabir.

Uganda imekuwa ni kati ya timu zinazoipa ushindani mkubwa Taifa Stars kwa muda mrefu licha ya Taifa Stars kuwa na kumbukumbu nzuri ya michezo miwili ya mwisho walipokutana katika kuwania kufuzu kwenda kushiriki Mashindano ya AFCON nchini Misri 2019. Taifa Stars ilitoka suluhu tasa dhidi ya Uganda katika mchezo wa kwanza uliopigwa (Septemba 08, 2018) ikiwa ugenini katika uwanja wa Taifa wa Uganda wa Nelson Mandela na baadaye kushinda kwa bao 3-0 kwenye mchezo wa marudiano uliopigwa kwenye uwanja wa Mkapa siku ya Jumapili ya Machi 24, 2019.