Uganda Yapata Pointi moja kwa Taabu Dhidi ya Wenyeji Tanzania
Mechi kati ya timu ya Beach Soccer ya Tanzania na Uganda imekuwa ni ya upinzani mkali kufuatia kila timu kukataa kufungwa na mpinzani wake.
Mechi hiyo imekuwa ni ya kusisimua kufuatia maandalizi bora yaliyofanywa na timu zote huku timu hizi mbili zikitoshana nguvu hadi dakika 36 za mchezo huo zinamalizika huku kila timu ikiwa na idadi ya mabao 3-3.
Baada ya matokeo kuwa pacha ndani ya muda wa kawaida zikaongezwa dakika 3 za nyongeza kama taratibu za Soka la ufukweni zinavyotaka ikiwa ni katika kutafuta mshindi; hata hivyo bado milango yote ikaendelea kuwa migumu licha ya kuongezwa kwa dakika hizo, ndipo ikalazimika kwenda kwenye mikwaju ya penati.
Uganda walifanikiwa kushinda kwa penati 2 huku Tanzania ikikosa penati zote na hivyo kuifanya Uganda kushinda na kujichukulia alama moja kwa kuwa mchezo wa Beach soka alama tatu hutolewa kwa timu inaposhinda ndani ya muda wa kawaida baada ya muda huo kuisha, basi mshindi hupewa alama 1 tu.
Waliopiga penati za Uganda na kupata walikuwa ni Byaruhanga Rica na Lwesibawa Godfrey huku Magwali Ronald akikosa; wakati kwa upande wa Tanzania waliopiga penati wakiwa ni Juma Sultan Ibrahim na Abdulkadir Ally Tabib ambapo wote hawakufanikiwa kujaza mpira kwenye nyavu.
Kocha wa Tanzania Boniface Pawasa amesema kuwa mechi ilikuwa ngumu, wachezaji wake wamepambana lakini bahati haikuwa kwao na pia Waganda waliwakamia sana katika mchezo huo huku akitoa malalamiko kwa waamuzi wa mchezo huo kwamba hawakuwa waungana.
Pawasa amesema wamekubali matokeo na kwamba watajipanga upya kwa michezo inayofuata kwa kuwa bado wana mechi 3, hivyo watajitahidi wapate alama zote tatu katika kila mchezo watakaocheza.
Naye Kocha wa Uganda Muwonge Salim Jamal amesema kuwa mchezo ulikuwa mgumu sana lakini wao walitegemea kuwa utakuwa wa namna hiyo kwa kuwa Tanzania ndio mabingwa watetezi wakajipanga kushinda na ndicho kilichotokea.
Wafungaji wa magoli kwa Tanzania ni Jaruph Juma na Stephano Wales Mapunda, huku goli la kwanza Likifungwa na Uganda kwa kujifunga wenyewe; kwa upande wa Uganda wafungaji ni Kasujji Davis na Lwesibawatimu Godfrey aliyepachika mabao 2 peke yake.
Mashindano hayo ya COPA DAR ES SALAAM yataendelea kesho (leo) katika viwanja vya Koko Beach.