VAR kwa mara ya Kwanza Kutumika Ligi Kuu U-20

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania TFF kwa mara ya kwanza limepanga kutambulisha teknolojia ya VAR kwenye mashindano ya ligi kuu ya vijana chini ya miaka 20 Julai 14, 2022 ambayo yamefikia kwenye hatua ya nusu fainali kwa msimu 21/22.

TFF imepanga kutambulisha teknolojia hiyo kwa lengo la kuwasaidia waamuzi katika kutatua baadhi ya changamoto ambazo huwa zinajitokeza wakati wa mechi, hususani yale makosa ambayo yanawapa wakati mgumu waamuzi kwenye kuamua.

Akizungumza kuelekea kwenye mechi mbili za nusu fainali meneja mashindano wa TFF Baraka Kizuguto alisema kuwa Shirikisho limeamua kufanya majaribio ya VAR kwenye mechi hizo kwa lengo la kuwasaidia waaamuzi kuweza kujiridhisha kabla ya kutoa maamuzi kwenye baadhi ya matukio.

“Sisi kama waendeshaji wa mashindano tumeona tunaendelea kukuwa na kubadilika kila msimu kwa kufanya vitu vipya ambavyo vinaweza kuwa bora zaidi na kuboresha mashindano yetu kuonekana kwenye ubora zaidi” alisema Kizuguto.

Mechi 2 za nusu fainali kutimua vumbi kesho Julai 14, 2022 ambapo mchezo wa kwanza utawakutanisha Coastal Union dhidi ya Mbeya Kwanza majira ya saa 9:00 alasiri na mchezo mwingine ukipigwa kati ya mabingwa watetezi wa ligi hiyo Mtibwa Sugar na Azam FC saa 12:00 jioni. Mechi zote zitapigwa kwenye uwanja wa Azam Complex Chamazi.