VPL KUENDELEA KESHO,MICHEZO MIWILI KUPIGWA

Ligi kuu ya Vodacom Tanzania VPL inaendelea kesho kwa michezo miwili kuchezwa kwenye Viwanja tofauti.

Uwanja wa Uhuru, Dar es salaam KMC FC wanawakaribisha Gwambina kutoka Mwanza.

Kocha wa KMC Habib Kondo, amesema mchezo utakuwa mgumu lakini wamejipanga vyema akiamini utakuwa bora zaidi kulinganisha na michezo iliyopita.

Naye nahodha Juma Kaseja amewatoa shaka mashabiki akisema licha ya kikosi chao kukosa wachezaji takribani watatu kwenye mchezo huo, wawili wakiwa majeruhi na mmoja akiwa anatumikia adhabu ya kadi nyekundu bado wanaamini watapata matokeo mazuri.

Kwa upande wake Kocha wa Gwambina Mohammedi Badru, amesema wamefanya maandalizi mazuri kuwakabili KMC na kupata matokeo yatakayo iweka timu yake mahali pazuri kwenye msimamo wa ligi.

Badru ameongeza kuwa licha ya ugeni wake katika kikosi hicho anaamini mbinu zake zitakuwa chachu ya matokeo mazuri wanayoendelea kuyapata.

Nahodha wa Kikosi hicho Paul Nonga amesema mchezo huo wanauchukulia ni wa kisasi wakikumbuka matokeo ya mchezo wa kwanza na wako tayari kuwakabili KMC.

Mchezo mwingine utachezwa uwanja wa Jamhuri, Dodoma ambapo Azam FC watakuwa wageni wa JKT Tanzania saa 10 jioni.