Waamuzi Mkafanye Kazi kwa Weledi
Makamu wa pili wa Rais TFF na Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi (TPLB) Steven Mnguto amewataka waamuzi kwenda kuyafanyia kazi kwa weledi mafunzo waliyopatiwa kwa kipindi chote cha semina, ikiwa ni pamoja na kupunguza lawama ambazo husababishwa na makosa ya kibinadamu.
Kauli hiyo ameisema Februali 22, 2022 wakati akifunga semina maalum ya wamuzi wanaotarajiwa kuchaguliwa kuchezesha mechi za mashindano ya Ligi ya Mabingwa wa Mikoa (RCL) iliyokuwa ikifanyika kwenye ukumbi uliopo Uwanja wa Benjamin Mkapa kwa siku 3 Februali 19 hadi Februali 22, 2022.
Mnguto alisema kuwa kundi kubwa linaloingia kwenye lawama ya mpira wa miguu ni waamuzi hasa ni kutokana na makosa ambayo yamekuwa yakijitokeza wakati wa michezo mbalimbali hasa katika kufanya maamuzi au kutoa maamuzi.
Alieleza kuwa fani ya uamuzi ni wito hivyo ni vyema kama waamuzi hao wataibeba hiyo na kwenda kufanyia kazi wito huo ambao kimsingi ni wao wenyewe walichagua kufanya bila ya shinikizo au kuagizwa na mtu yeyote.
Hata hivyo alielezea pia kuhusiana na mashindano hayo ya RCL kuwa ni kati ya mashindano ambayo yeye anaamini ni muhimu sana katika kuvumbuwa vipaji vya wachezaji kutoka katika hatua ya chini kabisa na hatimaye kuvipeleka juu, hivyo amewataka na waamuzi nao waichukue kama changamoto ama mahala ambapo wao pia wanapaswa kuonyesha uwezo wao katika kuchezesha mechi ili waweze kuchaguliwa katika mashindano mengine ya juu zaidi.
Kwa upande mwingine Mwenyekiti wa Kamati ya Waamuzi Nassoro Hamduni alisema kuwa kwa upande wao wanaimani kubwa kwa washiriki hao kwenda kufanya kazi kwa ufanisi wa hali ya juu kwenye majukumu yao kutokana na mafunzo ya utimamu wa akili na mwili kwa pamoja kwa siku zote hizo 3, na kwamba wanatarajia kuona mabadiliko makubwa kwa waamuzi hao hasa kuanzia katika mechi za RCL.
Naye moja kati ya washiriki hao Elizabeth Kessy akizungumza kwa niaba yaw engine alisema kuwa wamejifunza vitu vingi kwa siku zote 3 na kwamba wanaahidi kwenda kuyafanyia kazi yale yote waliyopatiwa na wakufunzi wao.
Semina hiyo iliyoandaliwa maalum kwaajili ya waamuzi watakao teuliwa kuchezesha mechi za mashindano ya Ligi ya Mabingwa wa Mikoa (RCL) ilijumuisha jumla ya washiriki 122 kutoka mikoa mbalimbali nchini, huku wakufunzi wakiwa ni Leslie Liunda, Israel Mujuni na Samuel Mpenzu.