Waamuzi wa First League, ligi kuu ya wanawake na RCL wapigwa Msasa
Semina ya siku tano ya waamuzi wa First league, ligi kuu ya wanawake na wanaochezesha ligi ya mabingwa wa mikoa (RCL) imefungwa leo Agosti 04,2022 na Makamu mwenyekiti wa kamati ya mashindano TFF James Mhagama katika uwanja wa Benjamini Mkapa jijini Dar es salaam.
Semina hiyo iliyojumuisha mafunzo ya nadharia na vitendo ilikuwa na lengo la kupitia changamoto zote zilizojitokeza msimu uliomalizika na kuzipatia suluhisho ili zisijitokeze tena katika msimu mpya unaotaraji kuanza Agosti 13, 2022. Lakini pia kuwaongezea ujuzi na maarifa wa kutekeleza majukumu yao wawapo uwanjani.
Akizungumza wakati wa kufunga semina hiyo makamu mwenyekiti wa kamati ya mashindano TFF James Mhagama aliwataka waamuzi hao kuongeza umakini katika kazi ili kupunguza makosa ya kibinadamu yanayojitokea mara kwa mara, lakini vilevile kutumia vyema maarifa waliyoyapata ili kuimarisha soka la Tanzania.
“Elimu ya darasani mliyoipata ikawasaidie katika kusimamia sheria za mpira lakini pia mnapotoka nje ya uwanja mkawe waadilifu na wenye maadili yanayofaa kwa kuwa ninyi ni kioo cha TFF watu wanapowatazama waone uadilfu ndani yenu. vishawishi ni vingi katika kazi yenu lakini nina imani kubwa kwamba mnaweza kuvishinda” alisema Mhagama.
Samweli Mpenzu mmoja kati ya wakufunzi wa semina hiyo alisema ana imani waamuzi wameyapata yote waliyotakiwa kuyapata ili ligi ya msimu huu iweze kuwa bora. Kiujumla asilimia 90% ya waamuzi wote wamefaulu lakini nafasi ziizopo ni chache hivyo waamuzi mna kazi ya ziada ya kuonyesha uwezo wenu katika kuchezesha ili kuweza kuzipata nafasi hizo.
Mbali na hayo mkufunzi huyo aliwataka waamuzi hao kutokuchagua aina ya mashindano ya kuchezesha wawe tayari kuchezesha mashindano yoyote kwa ngazi yoyote, hii itawapa wasaa wa wao kujipima na kupata uzoefu wa kufanya vizuri katika mashindano makubwa.
Akizungumza kwa niaba ya waamuzi wenzake Salma Chimbali kutokea Mtwara aliushukuru uongozi wa TFF kwa kuandaa semina hiyo ambayo imewajenga na wameweza kujifunza mambo mengi mapya hivyo watakwenda kuyafanyia kazi kwa vitendo.
.