Waziri Dkt.Pindi Chana: TFF inastahili pongezi

Waziri wa sanaa utamaduni na michezo Mheshimiwa Balozi Dkt.Pindi Chana Leo Februari 20, 2023 ametembelea kituo cha ufundi cha TFF kilichopo Kigamboni, Dar es salaam ikiwa ni ziara yake ya kwanza tangu ateuliwe kuwa Waziri wa wizara hiyo Februari 14, 2023.

Akizungumza mara baada ya kukamilisha ziara hiyo Waziri Chana alisema, TFF ina stahili kupongezwa kwa kazi kubwa ambayo wanaifanya katika maendeleo ya soka la Tanzania. Kumekuwa na mabadiliko makubwa sana katika soka Kwa kipindi kifupi cha uongozi wa Rais Karia katika kila sekta kuanzia Miundombinu, ubora wa timu za taifa, uzalishaji wa makocha wazaa na mengineyo.

“Leo nimeshuhudia miundombinu iliyopo katika kituo hiki cha kigamboni na hakika ni uwekezaji mkubwa ambao utaleta mageuzi makubwa katika soka. Nimeona viwanja viwili Bora hapa vya nyasi asili na bandia ambayo vitasaidia timu za taifa na timu nyinginezo lakini pia kuna sehemu nzuri za malazi pamoja na vyumba vya mafunzo hakika TFF inafanya kazi nzuri. Kama wizara tutaendelea kuwapa ushirikiano” alisema Mheshimiwa Waziri Chana.

Naye Rais wa TFF Wallace Karia alimshukuru waziri Chana Kwa kuona umuhimu wa kutembelea kituo cha ufundi cha Kigamboni na kuona miundombinu iliyopo ambayo itasaidia kukuza soka na kutoa mwaliko kwa Waziri huyo kufika katika kituo cha Tanga na kujionea uwekezaji mkubwa uliofanywa na TFF Kwa kushirikiana na FIFA. Hata hivyo Rais Karia alitoa rai kwa wadau na washirika mbalimbali wa michezo kuwekeza katika kituo hiko.

Katika ziara hiyo Waziri Chana aliambatana na Mkuu wa wilaya ya Kigamboni Mheshimiwa Halima Bulembo, Kaimu Mkurugenzi wa idara ya maendelezo ya michezo Ally Mayay, katibu mtendaji wa Baraza la Michezo (BMT) Bi. Neema Msita na viongozi wengine wa kiserikali.