Wizara Imewazawadia Fountain Gate Academy Milioni 10

Wizara ya Utamaduni, sanaa na Michezo imewazawadia timu ya Fountain Gate Dodoma wachezaji na benchi la ufundi fedha taslim shilingi Milioni 10 ikiwa ni sehemu ya pongezi baada ya timu hiyo kutwaa ubingwa wa Afrika kwenye fainali za African Schools Championship zilizofanyika Durban nchini Afrika Kusini.

Akizungumza wakati wa hafla fupi ya kuwapongeza iliyofanyika Aprili 11,2023 kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa, mgeni rasmi Waziri wa Utamaduni, sanaa na Michezo Balozi Dkt.Pindi Chana alisema kuwa Serikali kupitia Wizara hiyo imefurahishwa na kazi nzuri iliyofanywa na vijana hao na kwamba wameheshimisha Taifa kwa ujumla.

Dkt.Pindi aliongeza kuwa kwa kitendo cha timu hiyo kuleta Ubingwa nyumbani imetafsiri ya kwamba walikwenda kushiriki na kushinda na sitofauti na hapo, huku akiwataka wale wote waliotayari kuunga mkono juhudi za Mhe Rais Samia katika kupeleka mbele soka letu waweze kujitokeza kudhamini na kuwashika mkono vijana kwani milango iko wazi.

“Milango iko wazi kwa wale wote mnaotaka kuwafadhili karibuni sana tuweze kuona namna gani tunaendeleza soka hili muhimu” alisema Waziri

Hata hivyo kwenye hafla hiyo ambayo pia Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania Wallace Karia alihudhuria, naye alimuomba Waziri kutembelea kituo hicho cha Fountain na kile cha Alliance atakapo pata muda kutokana na vituo hivyo kuwa na mchango mkubwa wa kuzalisha vipaji vingi vya wachezaji kuanzia umri mdogo.

Rais Karia alisema kuwa kupitia vijana hao, Taifa lilifanikiwa kucheza fainali za kombe la Dunia U17 mwaka jana na kwamba kwa kutumia vijana hao na wengine wakiongezeka Taifa litafika tena Kombe la Dunia.

“Hawa na wengine tukiongezea tutafanikiwa kufika Kombe la Dunia, wakati wale waliocheza mwaka jana watakuwa wanaandaliwa kwaajili ya kushiriki Kombe la Dunia U20 yote hayo yapo kwenye mpango mkakati wetu”.Alisema Rais Karia

Timu ya Fountain Gate iliwasili hapa nchini Aprili 10,2023 ikitokea Afrika Kusini huku ikiwa pia imekusanya medali na tuzo mbalimbali walizo shinda kwenye fainali hizo.