WRCL Yapamba Moto Mwanza

Ligi ya Mabingwa wa mkoa kwa wanawake 2023 inayoendelea jijini Mwanza imeendelea kupamba moto kwa timu zote kutunishiana misuli vilivyo.

Ligi hiyo iliyoanza kutimua vumbi Julai 17,2023 imebakiza raundi moja kumalizika katika hatua ya makundi, ambapo kila timu itapaswa kuwa imecheza mechi 4 na nyingine zitacheza mechi 3 pekee kulingana na idadi ya timu kwenye kundi husika.

Mpaka sasa ni timu 3 pekee zilizocheza mechi zake zote kwenye hatua hiyo; kati ya timu 19, huku ikiwa Ziba Sekondari ndio timu pekee iliyojihakikishia kufuzu hatua ya Robo fainali. Timu nyingine zilizocheza mechi zake zote ni Singida Rising Stars na Kilimanjaro Wonders zote zikishindwa kupata alama za kuendelea kwenye michuano hiyo.

Hata hivyo, timu nyingine bado zimesaliwa na mchezo mmoja zaidi licha ya kuwa baadhi ya timu kama Mwanga City Queens, Gets Programm na Sayari Woman zimejihakikishia kufuzu hatua ya robo fainali.

Mechi nyingine za ligi kuhitimisha hatua ya makundi zitaendelea Julai 21, 2023; mechi zitachezwa kwenye uwanja wa Nyamagana na CCM Kirumba.