Yanga Princes Yawaonesha Ubabe Mlandizi Queens kwa Kuwanyuka Bao 2 Bila, Katika Uwanja wa Karume Leo

Mechi ya ligi kuu ya wanawake ya Tanzania Bara, kati ya ‘Yanga Princes’ na Mlandizi Queens imemalizika jioni ya leo tarehe 7 Desemba, 2019 katika uwanja wa Karume Jijini Dar es Salaam; ambapo timu ya Yanga Princes imeweza kuibuka na ushindi wa magoli mawili kwa bila.

Mchezo huo wa ligi kuu ya wanawake Bara ulianza  majira ya saa kumi jioni(10:00)  na ulikuwa wenye burudani ambapo timu zote mbili zilikuwa zikishambuliana kwa zamu.

Timu ya Yanga Princes ilifanikiwa kupata bao la kwanza katika dakika ya 37 mnamo kipindi cha kwanza, bao lililofungwa na mchezaji jezi namba 14 anayeitwa Shelda Boniface; bao lililodumu hadi timu zinakwenda katika mapumziko.

Kipindi cha pili, mpira ulianza kwa kasi kidogo huku Mlandizi Queens nao wakionesha kuhitaji kusawazisha goli hilo katika dakika za mwanzo za kipindi lakini ‘forward’ yao ilionekana kukosa umakini kidogo na hivyo kuifanya timu hiyo kushindwa kutumia nafasi ilizozipata katika kipindi hicho.

Mnamo dakika ya 53 Yanga Princes ilifanikiwa kuongeza bao la pili kupitia kwa mchezaji wake mwenye jezi namba 4, Amina Ally aliyepachika bao mardadi kabisa bao lililokamilisha idadi ya magoli 2 ya Yanga Princes na kufanya matokeo kubaki hivyo mpaka mwamuzi anapuliza kipyanga cha mwisho.

Kocha wa kikosi cha Yanga Princes,Nassoro Muhsini amesema kuwa kikosi chake kilijiandaa vema ili kushinda na kilicheza vizuri na kwa umakini mkubwa pia; na kwamba kocha  anatarajia kuendelea kufanya vema katika kila mchezo atakaocheza kwa kuwa amamalengo ya kutwaa ubingwa wa ligi hiyo ili kuandika historia kuwa kocha wa kwanza kutwaa kikombe cha kwanza cha ligi ya kwanza ya wanawake Tanzania Bara kwa msimu wa 2019/2020.

Ameeleza kuhusu maandalizi ya mchezo wake unaofuata dhidi ya Simba Queens na kusema  kuwa amejipanga kushinda kila mechi ili kuiweka timu yake katika nafasi nzuri kwenye ligi ya wanawake inayoendelea kuchezwa kwa mara ya kwanza hapa nchini Tanzania huku akibainisha kuwa lengo lake ni kutwaa ubingwa.

Naye kocha wa kikosi cha Mlandizi Queens, Ossieni Kioma amekubalina na matokeo hayo na kusema huo ndio mpira na matokeo hayo ni kawaida katika mchezo; na kudai kuwa ligi bado, kwani mpaka sasa amecheza mechi chache tu, hivyo bado anayo nafasi ya kupata matokeo mazuri kadri ligi inavyoendelea.

Vikosi vilivyocheza katika mechi hiyo kwa upande wa Yanga Princes ni: Belina Nyamwihuli(GK) (jezi 13), Happyness Mwaipaja (C-jezi 19), Mwantum Ramadhani(6), Fatuma Mwisendi (23), Fatuma Bushiri(24), Amina Ally(4), Asha Abduly(5), Nasma Khalid(7), Mwapewa Mtumwa(29), Shelda Boniface(14) Gresy Yusuph(10); huku wale wa akiba wakiwa: Tausi Swalehe(GK, jezi-30), Halima Kawaida(18),Zainabu Nienda(3), Aisha Juma(15)  Bahati Mwalami(11) na  Fausta Thomas jezi (17).

Wachezaji wa kikosi cha Mlandizi Queens walikuwa ni: Zainabu M. Abdallah(GK jezi namba 18), Mwanaisha Seif (15), Agness Kaloli(22), Hadija Mohamed(26) Shehati Mohammed (C-20), Rehema Mohamed (5), Milla Solly(12), Janeth Pangamwene(8), Jamila Hassani (14), Zainabu Pazzi(23) na Phiromina Kizima (7).     Wachezaji waakiba  ni: Rose Mrimi (11), Fatuma Mohamed  (9) na Anna Mwaisyula( 21).