Yanga Princess Ngoma Ngumu Kulisaka Taji (SWPL)

Mechi za Ligi Kuu ya Wanawake Serengeti Lite (SWPL) zimeendelea wiki hii, michezo mitano ikipigwa raundi ya 11 huku mambo yakionekana kuzidi kuwa magumu kwa Yanga Princess katika mbio za kulisaka taji la msimu huu wa ligi.

Mpaka sasa Yanga Princess ipo nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi kwa jumla ya alama 21 ikiwa imepoteza mechi 2, sare 3 na imeshinda michezo 6, wakati timu zinashuka dimbani kwenye raundi hiyo wenyewe Yanga walikuwa na kibarua cha kuikabiri Mkwawa Queens kule mkoani Iringa.

Hata hivyo mchezo huo ulioonekana kuwa na matokeo katiri kwa Yanga Princess kutokana na ubora walionao kulinganisha na wenyeji wao ulimalizika kwa suluhu tasa na kuifanya Yanga irudi Dar es salaam ikiwa na alama moja pekee baada ya kupoteza mbele ya Fountain Gate Princess kwenye mchezo uliopita.

Wakati Yanga Princess ikipitia wakati mgumu kabla ya kukutana na watani wake wa jadi Simba Queens kwenye mchezo unaofuata, upande wa pili huko wenyewe wanazidi kuipigilia misumari ngome yao ya kutetea taji baada ya kujipigia magoli 7-0  dhidi ya The Tiger kwenye mchezo uliopigwa Machi 14, 2023 uwanja wa Uhuru.

Simba Queens imeendelea kusalia kileleni kwa jumla ya alama 26, sawa na Fountain Gate Princess inayoshika nafasi ya pili baada ya kuongeza alama tatu ilizobeba kwenye uwanja wa nyumbani (Jamhuri) ilipo wakaribisha Amani Queens mchezo uliomalizika kwa matokeo ya 4-1.

Nafasi ya tatu imekaliwa na maafande JKT QUEENS baada ya ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Alliance Girls, matokeo mengine ni; 0-0 mchezo kati ya Ceasiaa Queens na Baobab Queens wenyewe wakifuatana kwenye msimamo wa ligi nafasi ya tano na ya sita.

Michezo mingine ya Ligi hiyo inatarajiwa kuendelea Machi 22, 2023 ikiwa ni raundi ya 12 ambapo itakuwa ndio raundi itakayo wakutanisha watani wa jadi kwenye mchezo wa marejeano msimu huu, huku wote wakiwa na kumbukumbu ya kupata sare kwenye mchezo wa duru ya kwanza.