Kikosi cha Yanga kimeanza vibaya katika Ligi Kuu Bara (Vodacom Premier League) baada ya kukubali kufungwa bao 0-1 dhidi ya Ruvu Shooting.

Dakika 20 Ruvu Shooting ilipata goli la kwanza kupitia kwa Sadat Mohamed baada ya beki wa Yanga, Kelvin Yondani kushindwa kumdhibiti vizuri Said Dilunga aliyetuliza mpira mbele yake na kupiga pasi iliyoenda kukutana na Sadat na kumuangalia kipa Faroukh Shikhalo na kuweka mpira moja kwa moja wavuni.

Yanga walitaka kusawazishq dakika 27, baada ya Papy Tshishimbi kuonganisha kwa kichwa krosi ya Patrick Sibomana na mpira ulitoka pembezoni kidogo mwa goli la Ruvu Shooting.

Licha ya Yanga kuwa nyuma kwa goli moja, Yanga walikuwa wakiutawala mchezo na kushambulia mara kwa mara langoni mwa Ruvu Shooting hali iliyowafanya mabeki wa timu hiyo kuwa na kazi ya ziada katika kuzuia.

Ushindi huo unawafanya Shooting kupata pointi tatu na goli moja huku Yanga wakitoka bila pointi yoyote katika mchezo huu.